Ukraine yahimiza dhamana ya usalama kabla ya mpango wa amani
3 Machi 2025Kauli ya Uingereza ya kuendelea kwa mazungumzo hayo ya kuandaa mpango wa amani katika mzozo wa Ukraine ambao utatakiwa baadaye kuwasilishwa kwa Marekani, imetolewa na msemaji wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Keir Starmer na kusisitiza kuwa mapendekezo mbalimbali yamewekwa mezani.
Kufuatia mkutano wa kilele wa mataifa ya Ulaya wa Jumapili mjini London, Ufaransa na Uingereza zilipendekeza usitishaji mapigano huko Ukraine kwa muda wa mwezi mmoja ambao ungepeleke kusitishwa kwa mashambulizi ya angani, baharini na kuilenga miundombinu ya nishati.
Hata hivyo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema usitishaji wowote wa mapigano bila ya kuwepo dhamana ya usalama, itakuwa ni ishara ya kushindwa kwa mchakato huo akisema hatua hiyo haitawezesha hatua ya kudumu ya kukomesha uvamizi wa Urusi.
Soma pia: Je, Marekani imewageuka washirika wake wa Ulaya na Ukraine?
Zelensky amepuuzilia mbali wazo la washirika wake kwamba kitendo cha kusitisha mapigano kitawezesha kuvimaliza vita hivyo huku akitabiri kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa Urusi itayavunja makubaliano hayo.
Kwa upande wake, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema ili Ulaya iweze kufanikisha mpango wa kudumu wa amani inapaswa kuwekeza zaidi kwenye ulinzi.
" Tunahitaji kuwa na nguvu kubwa ya ulinzi, hilo ni wazi kabisa. Tunataka amani ya kudumu, lakini amani hiyo ya kudumu inaweza tu kufikiwa kukiwepo na msingi imara. Na umadhubuti huo unatakiwa uanze kwa kujiimarisha sisi wenyewe. Hayo ndiyo madhumuni ya mpango wa ulinzi nitakayowasilisha kwa nchi wanachama kesho. Mpango wa kuwa na Ulaya iliyojiimarisha tena kwa silaha."
Dhamana ya usalama kwa Ukraine yazusha matatizo
Itakumbukwa kuwa suala hili la dhamana ya usalama ndilo liliibua majibizano makali siku ya Ijumaa kati ya rais Donald Trump wa Marekani na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky ambaye aliondoka katika Ikulu ya White House bila kutia saini mkataba wa awali wa kuiruhusu Marekani kuchimba madini adimu ya Ukraine, hatua iliyopelekea baadhi ya wanachama wa Republican kupendekeza kuwa Zelensky anapaswa kujiuzulu.
Soma pia: Zelensky asema yuko tayari kushirikiana na Marekani licha ya kuvutana na Trump
Mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa Marekani Mike Waltz amesema nchi hiyo inahitaji kiongozi ambaye anaweza kuwa tayari kushirikiana na Marekani na hata Urusi ili hatimaye kuvimaliza vita hivyo. Zelensky aliijibu kauli hiyo akisema haitakuwa rahisi kumpata atakayechukua nafasi yake, lakini akasema yuko tayari kujiuzulu ikiwa nchi yake itajumuishwa katika jumuiya ya kujihami ya NATO.
Mara kadhaa Urusi imekuwa ikisisitiza kuwa Zelensky sio kiongozi halali kwani angelitakiwa kufanya uchaguzi mwaka jana ikiwa nchi yake ingelikuwa na amani. Lakini, sheria ya kijeshi iliyotangazwa nchini Ukraine inapiga marufuku kufanyika kwa uchaguzi.
(Vyanzo: Mashirika)