Ukraine yadungua droni 90 zilizovurumishwa na Urusi
17 Machi 2025Jeshi la anga la Ukraine limesema mashambulizi ya droni za Urusi yaliyalenga miji ya Odesa, Kharkiv, Dnipropetrovsk, Kirovohrad, Sumy, Chernihiv. Mashambulizi hayo yalifanyika pia kwenye mji mkuu Kyiv. Jeshi limesema lilitumia vifaa vya kivita vya kielekroniki kuangusha droni zingine 70.
Gavana wa jimbo la Odesa, Oleh Kiper, amesema raia mmoja alijeruhiwa wakati wa shambulio hilo, ambalo liliharibu shule ya chekechea, nyumba ya makazi ya kibinafsi, duka na gari la abiria.
Kiper alisema takriban wakazi 500 katika vitongoji vya Odesa wameachwa bila umeme baada ya droni kuharibu miondombinu za nishati.
Soma pia:Zelensky: Urusi haionyeshi nia ya kuvimaliza vita
Kwa upande wake, Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema vikosi vyake vimechukua kijiji cha Stepove, Mkoani Zaporizhzhia, mashariki mwa Ukraine.
Pia wizara hiyo ya ulinzi aimesema katika taarifa tofauti kwamba jeshi lakeliharibu droni 72 za Ukraine kwenye anga yake. Droni nizo nipamoja na 36 kwenye eneo la Kursk maharibi mwa Urusi.
Trump kuzungumza na Putin
Rais wa Marekani Donald Trump anapanga kufanya mazungumzo na kiongozi mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin kesho Jumanne. Trump amesema mazungumzo hayo yanahusu juhudi za kuvimaliza vita vya Ukraine.
Trump amesema mazungumzo tayari yanaendelea kuhusu kugawanya mali kadhaa kati ya pande hizo hasimu. Kulingana na Trump, ardhi na mitambo ya kufuwa umeme ndiyo kiini cha mazungumzo ya kufikia amani kati ya Urusi na Ukraine.
Maafisa wa Marekani walielezea matumaini yao kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Ukraine na Urusi yanaweza kufikiwa katika wiki chache zijazo.
Soma pia:Starmer: Putin hana budi kuketi kwenye meza ya mazungumzo
Hapo awali, Moscow ilisema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alikuwa na mazumgumzo ya simu na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov kujadili "mambo madhubuti ya utekelezaji wa makubaliano" kati ya Urusi na Ukraine.
Hata hivyo, Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amemuomba Donald Trump kutofanya makubaliano ya upande mmoja na Vladimir Putin ambayo inaweza kuidhuru Ukraine.
Akizungumza leo Jumatatu katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Baerbock alisisitiza umuhimu wa umoja nchi za Magharibi, akisisitiza kwamba hadhi ya Ukraine lazima ibaki kuwa msingi wa mazungumzo yoyote.
Mataifa mengi ya Umoja wa Ulaya yanaonesha wasiwasi wake kuhusu mbinu ya Trump katika kufikia makubaliano ya amani baina ya Ukraine na Urusi, ikiwa ni pamoja na shinikizo kwa Ukraine kuachana na mpango wake wa kujiunga na jumuiya ya kujihami ya NATO.