Urusi yashambulia kwa droni vituo vya nishati vya Ukraine
31 Agosti 2025Hayo ni kwa mujibu wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliyeapa kulipiza kisasi kwa kuamuru mashambulizi zaidi ndani ya ardhi ya Urusi. Kampuni kubwa kabisa ya kibinafsi ya nishati nchini Ukraine, DTEK, imesema droni za Urusi zilivishambulia usiku vituo vinne vya nishati katika mkoa wa Odesa. Mamlaka za eneo hilo zimesema watu 29,000 walikuwa bila umeme mapema leo.
Mjini Vatican, Kiongozi wa kanisa katoliki Papa Leo ametoa wito wa kusitishwa mapigano. Amesema katika maombi yake na mahujaji kwenye Ukumbi wa Mtakatifu Petro kuwa ni wakati wa wale wanaohusika kuweka chini silaha na kutumia njia ya mazungumzo na amani kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa. Miaka mitatu na nusu baada ya kuanza vita, Urusi na Ukraine zimeimarisha mashambulizi yao ya anga katika wiki za karibuni. Urusi imekuwa ikiilenga mifumo ya nishati na usafiri ya Ukraine, wakati Ukraine ikishambulia vinu vya kusindika mafuta na mabomba ya Urusi.