Ukraine, Ulaya wana matumaini na mkutano wa Trump na Putin
14 Agosti 2025Ukraine na washirika wake wa Ulaya wameashiria matumaini kwamba Rais wa Marekani Donald Trump atashinikiza kusitishwa kwa vita, katika mazungumzo na Rais Vladimir Putin wa Urusi kesho Ijumaa bila kuisaliti Ukraine au kupendekeza kugawa eneo lake.
Viongozi wa Ulaya na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, hapo jana walifanya mkutano kwa njia ya mtandao na Trump, kuelekea mazungumzo ya kesho yanayosubiriwa kwa shauku kubwa huko Alaska.
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz aliyekuwa mwenyeji wa mkutano huo, alisema Trump na Ulaya wako tayari kuongeza shinikizo kwa Urusi ikiwa siku ya Ijumaa mazungumzo hayatokuwa na mwafaka.
Kulingana na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Rais Trump amekubali kwamba Ukraine ni lazima ishirikishwe katika majadiliano yoyote kuhusu kugawa ardhi huku Zelensky akisema Trump aliunga mkono wazo la hakikisho la usalama katika suluhisho la baada ya vita.