Ukraine, Ulaya na Trump waungana kabla ya mkutano na Putin
14 Agosti 2025Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema Ukraine, washirika wake wa Ulaya na Rais wa Marekani Donald Trump wamekuwa na mwelekeo wa pamoja kabla ya mkutano uliopangwa kufanyika kati ya Trump na Rais wa Urusi Vladimir Putin huko Alaska siku ya Ijumaa.
Kiongozi huyo wa Ujerumaniameeleza kuwa kuna ulazima wa kulindwa kwa "maslahi ya msingi ya usalama wa Ulaya na Ukraine" katika mazungumzo hayo ya Alaska. Zaidi ameelezea vipengele muhimu katika upatikanaji wa makubaliano ya amani na Urusi.
"Tumeweka wazi mambo mbalimbali kwa ajili ya mazungumzo hayo. Tumesema uwazi kwamba Ukraine lazima iwe mezani mara tu vikao vya ufuatiliaji vitakapofanyika. Tunataka mazungumzo yaendelee kwa utaratibu unaofaa. Usitishaji mapigano lazima uwe kipaumbele. Ukraine iko tayari kujadiliana juu ya masuala ya kimaeneo. Hata hivyo kile kinachoitwa njia ya mawasiliano, iwe ndio mahali pa kuanzia na utambuzi wa ukaliaji wa Urusi hauwezi kujadiliwa. Kanuni ya kwamba mipaka haiwezi kubadilishwa kwa nguvu lazima iendelee kutumika."
Merz, Zelensky na baadhi ya viongozi wa Ulaya walifanya mazungumzo kwa njia ya video na Trump na Makamu wake wa Rais JD Vance kuhusu mkutano wa Ijumaa ambao unasubiriwa kwa shauku kubwa katika kutafuta mwafaka wa vita vya Urusi nchini Ukraine. Mazungumzo hayo yalipangwa kwa muda mfupi na Kansela Merz, huku Zelensky akisafiri hadi mjini Berlin kuhudhuria moja kwa moja mazungumzo hayo.
Kabla ya mazungumzo na Trump, Zelensky alijiunga na mkutano wa awali pia kwa njia ya video kati ya viongozi wa Ulaya ambao ulijumuisha viongozi kutoka Ufaransa, Uingereza, Italia, Poland na Finland, pamoja na Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, Rais wa Baraza la Ulaya António Costa na Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte.
Ulaya, Zelensky kuzungumza na Trump kabla ya mkutano na Putin nchini AlaskaZelensky amewaeleza viongozi wa Ulaya kwamba Rais Putin "haonyeshi nia ya kweli" kuhusu kumaliza vita vya Ukraine, akiongeza kuwa Putin anajaribu kuonyesha kuwa Urusi ina "uwezo wa kuidhibiti Ukraine nzima", na kupuuzia vikwazo "kana kwamba havifanyi kazi na havina tija", jambo ambalo Zelensky amedai kuwa si kweli kwani vikwazo hivyo vinaathiri uchumi wa Moscow.
"Tulizungumza juu ya mkutano huko Alaska. Tunatumai kuwa mada kuu ya mkutano huo itakuwa usitishaji wa mapigano mara moja, na rais wa marekani amerudia kusema hivi. Alipendekeza kwangu kwamba baada ya mkutano huko Alaska tutakuwa na mazungumzo na tutajadili matokeo yote, ikiwa kuna lolote. Na tutaamua hatua zinazofuata za pande zote."
Kulingana na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Rais Trump wa Marekani "ameweka wazi" katika mkutano huo kwamba Washington inalenga kufanikisha makubaliano ya usitishaji vita katika mkutano wa kilele na Rais Putin huko Alaska. Macron aliongeza kuwa Trump amekuwa wazi kwamba "masuala ya kimaeneo yanayohusiana na Ukraine yatajadiliwa tu na rais wa Ukraine".
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz alikuwa ameitisha mikutano hiyo kwa njia ya mtandao kujaribu kuhakikisha viongozi wa Ulaya na Ukraine wanasikilizwa kabla ya mkutano wa Alaska. Kremlin:Mkutano wa Putin na Trump utakuwa wa manufaa makubwa kuelekea amani ya kimataifa
Baada ya mkutano huo, Rais Trump alitoa onyo kwa Putin kuwa atakabiliwa na "hatua kali" ikiwa hatakubali kumaliza vita nchini Ukraine. Trump alisema kuwa Putin anapaswa kujiandaa kwa hili ikiwa hatakubali kusitisha vita wakati wa mkutano wao wa Ijumaa katika mji huko Alaska nchini Marekani.
Kiongozi huyo pia amedokeza kwamba atajaribu kufanya mkutano wa pande tatu na kuwakutanisha Zelensky na Putin mara moja mara baada ya mazungumzo ya Alaska.