Trump 'anaishi katika dunia ya upotoshaji', asema Zelensky
19 Februari 2025Hayo ni wakati mzozo wa Ukraine na Urusi ukionekana kuchukua mkondo tofauti kufuatia mazungumzo yaliyofanywa kati ya wanadiplomasia wa Marekani na Urusi mjini Riyadh.
Akizungumza na waandishi habari Jumanne, Trump aliunga mkono hoja nyingi za Urusi kuhusu vita vya nchini Ukraine, akilaumu Kyiv kwa "kuanzisha" mapigano na kuashiria kuwa Zelensky hana umaarufu sana. Trump alidai kuwa rais mwenzake wa Ukraine ana kiwango cha chini sana cha uungaji mkono nchini mwake – licha ya tafiti za maoni kuonesha tofauti.
Moscow inawapotosha Wamarekani
Zelensky amejibu, akiituhumu Urusi kwa kuwapotosha Wamarekani, "Kwa bahati mbaya, Rais Trump, ambaye tunamheshimu sana kama kiongozi wa watu wa Marekani, ambaye tunamheshimu sana, ambaye anatuunga mkono kila wakati, kwa bahati mbaya anaishi katika dunia ya upotoshaji."
Kauli hizo zinafutia ripoti kuwa Urusi na Marekani ilijadili uwezekano wa kufanyika uchaguzi nchini Ukraine, wakati wa mazungumzo ya ngazi ya juu mjini Riyadh, jana. Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na waziri mwenzake wa Urusi Sergey Lavrov walibadilishana mawazo kuhusu suala hilo lakini akaongeza kuwa uamuzi hauwezi kufanyika Moscow au Washington.
Aidha Zelensky amesema kuwa anaamini Marekani imemsaidia rais wa Urusi Vladmir Putin kuondokana na kutengwa kwa miaka mingi na nchi za Magharibi.
Mjumbe wa Trump kuhusu Ukraine yuko Kyiv
Wakati huo huo, mjumbe maalum wa Trump kuhusu Ukraine, Keith Kellogg, aliwasili katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev leo asubuhi katika kile alichosema ni ziara ya kukaa na kusikiliza hoja za Kyiv.
"Nadhani ni kuhusu tutakachokisikiliza. Tunaelewa haja ya kuhakikishiwa usalama. Ni wazi kwetu hili ni taifa lenye uhuru wake. Na sehemu ya dhamira yangu ni kuketi na kusikiliza na kusema, "Nini kero zenu?"
Zelensky amesema anatumai Kellogg ataitumia ziara yake Kyiv kujionea hali ilivyo ili kubaini ukweli. Ukraine imekuwa chini ya sheria ya kijeshi tangu Urusi ilipofanya uvamizi kamili, na ikaahirisha uchaguzi wa rais na bunge na kusitisha shughuli za kisiasa. Vita vya Urusi na Ukraine vinaingia mwaka wake wa nne wiki ijayo.
Mjini Moscow, Rais Putin amesema leo kuwa anayaweka mazungumzo kati ya Marekani na Urusi yaliyofanyika Saudi Arabia "kwenye kiwango cha juu", na kuyataja kama "hatua ya kwanza" ya kurejesha uhusiano na Washington.
afp, dpa, reuters, ap