Mashambulizi ya droni yarindima tena Ukraine na Urusi
15 Machi 2025Ukraine imesema droni nyingine 38 zilizorushwa na Urusi zilipoteza mwelekeo. Jeshi la nchi hiyo limeongeza kuwa Urusi ilifanya pia mashambulizi mawili ya makombora.
Kampuni binafsi kubwa zaidi ya umeme ya Ukraine DTEK imesema mashambulizi hayo yameharibu miundombinu yake ya umeme katika mikoa ya Dnipropetrovsk na Odesa. Imeongeza kuwa madhara yaliyojitokeza ni makubwa na kuwa baadhi ya watu katika maeneo hayo sasa hawana umeme.
Soma zaidi: Ukraine kuimarisha ulinzi kufuatia ongezeko la mashambulizi ya Urusi
Kwa upande wake Urusi imesema imeziangusha droni 126 za Ukraine usiku wa kuamkia kwenye mikoa ya Voronezh, Belgorod, Bryansk, Rostov na Kursk. Nchi hizo jirani zimeshambuliana katika muda usiopungua saa 24 tangu Rais wa Urusi Vladimir Putin alipokutana na mjumbe wa Marekani Steve Witkoff kujadili pendekezo la Marekani la kusimamisha vita kwa siku 30 nchini Ukraine.
Katika hatua nyingine, Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema imefanikiwa kuvikomboa vijiji viwili katika mkoa wa Kursk. Urusi imeongeza kasi ya kuwafurusha wanajeshi wa Ukraine walioteka sehemu ya mkoa wa Kursk walipofanya uvamizi wa ghafla mwezi Agosti mwaka uliopita.