Ukraine na Marekani wajadili mpango wa kusitisha vita
11 Machi 2025Ukraine imewasilisha mpango wake wakusitisha kwa sehemu mapigano na Urusi ukiwasilishwa saa chache baada ya Ukraine kufanya mashambulizi yake makubwa zaidi ya rubani dhidi ya Urusi ndani ya miaka mitatu ya vita.
Ukraine inatarajia kuwa mpango huo wa kusitisha kwa sehemu mashambulizi ya anga na baharini utaishawishi Marekani kurejesha msaada wake kwa nchi hiyo.
Mkuu wa ofisi ya rais nchini Ukraine, Andriy Yermak, amewaambia waandishi wa habari kwamba wako tayari kufanya wawezavyo kufikia amani.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Marco Rubio, na mwenzake wa Ukraine, Andriy Sybiga, walihudhuria mkutano huo wa Jeddah ambao Urusi haikushiriki huku Rais Donald Trump akiongeza shinikizo kwa Ukraine kumaliza vita vilivyoanza kwa uvamizi wa Urusi wa mwaka 2022.