Ukraine kuwasilisha mpango wa kusitisha vita kwa Marekani
11 Machi 2025Mkutano huo utakaofanyika baadaye leo kati ya maafisa wa Ukraine na Marekani katika mji wa bandari wa Jeddah, nchini Saudi Arabia, utakuwa wa maafisa wa ngazi za juu zaidi tangu ziara iliyotibuka ya Rais Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya White House mwezi uliopita wakati Trump alipomshtumu kiongozi huyo wa Ukraine kwa madai ya kukosa shukrani.
Zelensky alikuwa Jeddah jana kukutana na watawala wa Saudi Arabia lakini hakushiriki katika mazungumzo yaliyohudhuriwa na maafisa wake watatu wa ngazi za juu.
Kabla ya mkutano huo wa leo, Ukraine imefanya mashambulizi katika kile ambacho meya wa Moscow, Andrei Vorobyov, amekielezea kuwa shambulizi kubwa la usiku kucha huku droni 337 zikidunguliwa kote nchini humo na 91 katika mji huo mkuu wa Urusi.
Vorobyov amesema shambulizi hilo lilisababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhiwa kwa wengine tisa.