Ukraine kupokea ahadi mpya za misaada Paris
27 Machi 2025Haya yanafanyika wakati ambapo Rais Volodymyr Zelenskiy ameitaka Marekani kutoyakubali matakwa ya Urusi katika vita vya Urusi vilivyodumu kwa miaka mitatu nchini Ukraine.
Mkutano huo wa tatu wa kilele ambao Ufaransa imeuita muungano wa "wenye nia na wanaoweza" unawaleta pamoja viongozi kama Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mark Rutte, Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni na Makamu wa Rais wa Uturuki Cevdet Yilmaz.
Yuro bilioni 2 kama msaada kwa Ukraine kutoka Ufaransa
Katika kikao na waandishi wa habari alichokifanya pamoja na Rais Zelenskiy usiku wa kuamkia Alhamis, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameelezea haja ya Ukraine kuendelea kusaidiwa.
"Tunastahili kuendelea kuisaidia Ukraine kwasababu ni muhimu kuendelea kupambana na mashambulizi ya Urusi. Leo natangaza msaada wa ziada wa kijeshi wa yuro bilioni mbili kutoka Ufaransa kwa ajili ya Ukraine," alisema Macron.
Zelenskiy amesema mbali na huo msaada wa Ufaransa, washirika wengine wa Ukraine wanaweza kutangaza misaada yao Alhamis. Kwa kuwa Marekani haitokuwa kwenye mkutano huo wa kilele, maafisa wa Ufaransa wanasema matokeo yake yatawasilishwa kwa utawala wake pia.
Mazungumzo katika mkutano huo yatajikita katika kuiimarisha Ukraine kijeshi ili kuzuia mashambulizi ya baadae na jinsi ya kuangalia usitishwaji wa mashambulizi katika shabaha za baharini na miundo mbinu ya nishati, kama ilivyojadiliwa katika mazungumzo yanayoongozwa na Marekani wiki hii nchini Saudi Arabia.
Maafisa wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, juhudi za Ulaya zinazoongozwa na Macron na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer kwa ajili ya kubuni mipango ya usalama kwa Ukraine zinahamia kutoka kwenye kutuma vikosi vya kijeshi na kuzingatia mbadala, kwa kuwa wanakabiliwa na vizingiti vya kisiasa na kimkakati, na uwezekano wa Marekani na Urusi kupinga mipango yao.
Waraka wa mkutano huo ulioonekana na Reuters unaonesha kwamba kutakuwa na mpango wa kuunda kikosi kitakachokuwa nchini Ukraine mbali na mstari wa mbele wa mapigano, kama sehemu ya makubaliano ya baadae ya amani yatakayoungwa mkono na Marekani. Kikosi hicho kitakuwa na jukumu la kuhakikisha usalama na kuzuia uvamizi wa baadae wa Urusi.
Korea Kaskazini imetuma vikosi 3,000 zaidi kwa Urusi
Hayo yakiarifiwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema anaitaka Marekani na washirika wengine wa Ukraine kutoka nchi za Magharibi, kutokubaliana na matakwa ya Urusi katika vita vinavyoendelea.
Zelenskiy amesema Urusi imeweka matakwa mengine ya ziada kwa ajili ya kutekelezwa kwa mkataba wa amani katika Bahari Nyeusi na miundo mbinu ya nishati, ikilenga kupunguzwa kwa shinikizo la vikwazo ilivyowekewa.
Rais huyo wa Ukraine amesema kauli za Marekani za kuiunga mkono Urusi, zinadhoofisha shinikizo kwa Urusi na juhudi za kuleta amani katika mzozo huo mkubwa wa Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia.
Wakati huo huo, jeshi la Korea Kusini limesema Korea Kaskazini imetuma kikosi cha majeshi 3,000 zaidi mwaka huu pamoja na makombora na silaha zengine kuisaidia Urusi kupambana na Ukraine.
Urusi na Korea Kaskazini hazijathibitisha taarifa hizo ila mataifa hayo mawili yalisaini mkataba wa kijeshi mwaka jana, Rais Vladimir Putin alipofanya ziara ya nadra Korea Kaskazini.
Vyanzo: Reuters/AFP