Ukosoaji waongezeka hujuma za Israel huko Gaza
22 Julai 2025Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa Jean-Noël Barrot amelaani kwa matamshi makali leo Jumanne uamuzi wa Israel wa kutanua hujuma zake za kijeshi kwenye Ukanda wa Gaza ikiulenga mara hii mji wa Deir al-Balah.
Mwanadiplomasia huyo amekiambia kituo kimoja cha redio nchini Ufaransa kuwa hali ya kibinadamu kwenye Ukanda wa Gaza "inafedhehesha" na ameitaja kuwa "kashfa kubwa" kwa Israel na Jumuiya ya Kimataifa.
Amesema "hakuna sababu yoyote hivi sasa inayoweza kuhalalisha mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza" na amelaani vikali matendo yanayofanywa na jeshi la nchi hiyo yanayowalazimisha mamia kwa maelfu ya Wapalestina "kuishi maisha dhiki na balaa."
Siku chache zilizopita Israel ilitangaza kutanua operesheni zake za kijeshi kwenye wa Deir al-Balah, ambao ndio pekee haujashuhudia mashambulizi makali ya nchi hiyo tangu vita vilipoanza zaiid ya miezi 21 iliyopita.
Watawala mjini Tel Aviv wamesema wanashuku kundi la Hamas linawashikilia mateka wengi wa Israel kwenye mji huo.
Wamedai operesheni yao ya ardhini kwenye mji huoinanuwia kuongeza mbinyo kwa kundi la Hamas liwaachie mateka na liweke chini silaha.
Hata hivyo mashambulizi hayo yamesababisha ukosoaji mkubwa wa kimataifa ikiwa ni pamoja na kutoka kwenye mataifa yanayozingatiwa kuwa washirika wakubwa wa Israel.
Uingereza yatishia vikwazo zaidi dhidi ya Israel
Hii leo mwanadiplomasia mwingine wa nchi ya Ulaya ameionya Israel kuwa itakabiliwa na vikwazo zaidi iwapo haitokubali kusitisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza David Lammy amesema "amefadhaishwa" na "kukasirishwa" na matendo ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.
Ameukosoa mfumo wa usambazaji misaada ya kiutu unaosimamiwa na Israel akiutaja kuwa "usio na utu" huku akisema matendo ya Israel yanaipaka tope nchi hiyo mbele ya macho ya walimwengu.
"Ninaamini kwa dhati kabisa kwamba matendo ya serikali ya Israel yanaichafulia jina Israel kwa kiwango kisichosemeka mbele ya ulimwengu na kuuweka rehani usalama wa Israel kwa muda mrefu unaokuja. (Benjamin) Netanyahu ni lazima awasikilize watu wa Israel, ambao asilimia 82 wanataka usitishaji mapigano na (hata) familia za mateka zinaamini hiyo ndiyo nafasi nzuri zaidi ya kuwarejesha nyumbani wapendwa wao." amesema Lammy.
Matamshi hayo ya Lammy na Barrot yanafuatia barua ya wazi iliyochapishwa jana Jumatatu na kutiwa saini na mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi 24 nyingi zikiwa Ulaya kulaani matendo ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.
Israel ´yatia pamba masikio´ operesheni yake Deir al-Balah
Licha ya ukosoaji wote huo Israel imeendelea kuushambulia mji wa Deir al-Balah na alfajiri ya leo Jumanne wingu zito la moshi lilionekana kwenye anga ya mji huo baada ya jeshi la Israel kuvurumisha makombora.
Maafisa wa afya wa Gaza wanasema watu 15 wameawa tangu usiku wa manane.
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO limesema vituo vyake kadhaa vimeshambuliwa kwenye mji huo na mkuu wa shirika hilo Tedros Adhanom Ghebreyesus amelaani hujuma hizo.
Amesema wanajeshi wa Israel walivamia vituo vya WHO na kuwalazimisha wanawake na watoto wanaondoke kwa miguu kuelekea mji mdogo jirani wa Al-Mawasi.
Ameongeza kuwa wafanyakazi wanaume wa shirika hilo na familia zao walifungwa pingu na kuvuliwa nguo karibu ya kuwa uchi na kuhojiwa kwa lazima na kupekuliwa chini ya mtutu wa bunduki na hadi sasa bado wanashikiliwa.