Ukosoaji dhidi ya Israel waongezeka kwa vitendo vyake Gaza
25 Julai 2025Mara tu baada ya tangazo la Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa aliyeandika siku ya Alkhamis (24 Julai) kupitia mtandao wa X kwamba nchi yake ingelitambua rasmi taifa la Palestina kwenye Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa mnamo Septemba, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alijibu kwa ukali tamko hilo akisema "ni sawa na kuwazawadia magaidi".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, aliita hatua hiyo ya Ufaransa isiyo na maana yoyote zaidi ya "kurejesha nyuma juhudi za kupatikana kwa amani ya kudumu" kwenye mzozo huo wa Mashariki ya Kati.
Kwa upande mwengine, Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, amejikuta kwenye shinikizo kali kutoka kwa wabunge wanaomtaka atangaze haraka kuitambua Palestina kama taifa huru, huku mwenyewe akisema mkwamba hali ya kibinaadamu inayoendelea kwenye Ukanda wa Gaza kwa saa "haisemeki wala haiwezi kutetewa."
Starmer alisema kwamba utaifa ni "haki isiyoepukika" kwa watu wa Palestina ingawa alisisitiza kwamba usitishaji mapigano lazima liwe jambo la awali.
"Nitakuwa na mkutano na washirika wetu kesho, ambapo tutajadiliana kipi tunachoweza kufanya kwa haraka kuzuwia mauaji na kuwapatia watu chakula wanachokihitaji kwa haraka sana, huku tukichukuwa jitihada zote kupata amani ya kudumu." Alisema waziri mkuu huyo wa Uingereza.
Gauck aikosowa Israel
Sauti ya ukosoaji dhidi ya Israel ilitolewa pia na rais wa zamani wa Ujerumani, Joachim Gauck, ambaye aliita operesheni ya kijeshi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza kama "iliyochupa mipaka" na "ya ovyo kabisa."
Akizungumza na kituo cha televisheni cha ZDF siku ya Alkhamis, Gauck alisema kusababisha mateso yasiyosemeka kwa "watu wengi wasiokuwa na hatua kwa lengo la kumuadhibu mwenye makosa, ni jambo la ovyo kabisa kwa sababu halina kipimo."
Hata hivyo, Gauck aliyehudumu kwenye nafasi ya urais wa Ujerumani kutoka mwaka 2012 hadi 2017, alisema daima amekuwa akijihisi kuwa na mahusiano binafsi na mapenzi kwa Israel, ambayo hayawezi kumtoka moyoni.
Utapiamlo waongezeka Gaza
Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka (MSF) lilisema siku ya Ijumaa (Julai 25) kwamba robo ya watoto na wanawake wajawazito au wanaonyonyesha waliochunguzwa kwenye Ukanda wa Gaza ndani ya kipindi cha wiki chache zilizopita wamegundulika kuwa na utapiamlo, likiituhumu Israel kwa kile lilichokiita "sera ya kuwauwa watu kwa njaa."
Idadi ya Wapalestina waliokwishakuuawa tangu vilipoanza vita mnamo Oktoba 2023 imefikia 59,587, huku wengine 143,498 wakijeruhiwa, kwa mujibu wa mamlaka za afya za Gaza.
Ndani ya masaa 24 yaliyopita, operesheni za Israel kwenye Ukanda huo zimewauwa watu 89 na kuwajeruhi wengine 435, ambapo 23 ya waliouawa walikuwa kwenye maeneo ya kupokea misaada ya chakula.