Ukosefu wa ajira kwa vijana nchini Afrika Kusini
21 Mei 2025Katika mitaa ya miji mikubwa hapa Afrika Kusini, sauti za matumaini kwa vijana wengi zimeanza kufifia. Kila alfajiri huamka wakiwa na matumaini mapya, lakini mchana ukifika, matumaini hayo huzama kama jua la jioni. Takwimu za hivi karibuni kutoka StatsSA zinaonesha kuwa zaidi ya vijana milioni 4.8 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 34 hawana ajira. Kwa wengi, si tu ukosefu wa kipato bali ni kukosekana kwa sababu ya kuishi.
Sello Kubele, kijana asiye na kazi katika mitaa ya Mamelodi nje kidogo ya jiji la Pretoria, anaeleza namna walivyochoka kusubiri msaada wa serikali.
Kiwango cha ukosefu wa ajira Afrika Kusini kimeongezeka hadi asilimia 32.9
“Tunajitengenezea ajira zetu wenyewe, unajua. Serikali, chama cha ANC, wameshindwa kutupatia ajira, hivyo tumeamua kujiundia ajira sisi wenyewe. Lakini bado ni yaleyale. Tunapojaribu kuhangaika mitaani kutafuta riziki, bado wanatufukuza, ilhali hawatupatii ajira,” alisema Sello Kubele.
Matukio kama haya sio machache. Vijana wengi wanakumbwa na msongo wa mawazo, wasiwasi, na hata wanawaza kujiua.
Ukosefu wa ajira kwa vijana sio tu tatizo la kiuchumi bali pia janga la afya ya akili
Kwa mujibu wa Tiyani Mohlaba, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa asasi isiyo ya kiserikali ya Afrika Tikkun inayojihusisha na maendeleo ya watoto na vijana katika jamii zenye changamoto humu nchini, ukosefu wa ajira kwa vijana si tatizo la kiuchumi tu, bali pia ni janga la afya ya akili.
"Baadhi yao huishia kuacha masomo kabisa… wanaporudi kupitia programu zetu, mara nyingi huwa na matatizo makubwa ya afya ya akili, mawazo ya kujiua, ukosefu wa ujuzi wa kuwasiliana, na mara nyingine hujihusisha na vurugu," aliongeza kusemma Tiyani Mohlaba.
Watoto milioni 72 watumikishwa Afrika
Ripoti ya hivi karibuni kutoka kwa idara ya StatsSA kuhusu ajira, ikiwa ya kwanza tangu Rais Cyril Ramaphosa achaguliwe kwa muhula wake wa pili, imeibua mashaka kuhusu utekelezaji wa ahadi za serikali. Ripoti hiyo imeonyesha hali tofauti na ile aliyoahidi wakati wa kampeni, ambapo alieleza kuwa serikali ingewekeza mabilioni ya pesa ili kuwapa wananchi ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
“Tutatumia pia kiasi kikubwa cha fedha mabilioni kwa ajili ya kuwafundisha watu kupata ujuzi, ujuzi unaoweza kutumika vyema katika uchumi wetu, kwa sababu lengo letu ni kuunda ajira zenye ubora," Cyril Ramaphosa.
Ukosefu wa ajira kwa vijana nchini Afrika Kusini unaathiri sio tu hali zao za kiuchumi bali pia afya yao ya akili. Ingawa serikali imeahidi kuwekeza katika mafunzo ya ujuzi, changamoto bado ni kubwa na vijana wengi wamepoteza matumaini. Ni muhimu hatua za haraka zichukuliwe ili kuwasaidia vijana kabla hawajakata tamaa kabisa.