Ujerumani yatoa wito kwa vijana wajiunge na jeshi
11 Aprili 2025Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius, serikali inasubiri tu kukamilika kwa taratibu za kisheria, ili ianze usajili na mafunzo kwa sehemu ya kwanza ya makuruta wapya 5,000 wanaotazamiwa kujiunga mwaka huu.
Mwanasiasa huyo kutokea chama cha Social Democrat, SPD, amesema kazi ya awali tayari imeshakamilika kwa miezi kadhaa sasa, na hivyo kuziwezesha hatua nyengine kufuata mara tu serikali mpya itakapoanza kazi.
Usajili wa vijana jeshini uko chini ya makubaliano ya uundaji wa serikali ya mseto ya Ujerumani
Makubaliano ya uundaji wa serikali ya mseto kati ya SPD na muungano wa vyama vya kihafidhina vya CDU-CSU yanataka uanzishwaji wa mfumo wa usajili wa jeshini, ambao katika hatua za awali utakuwa wa hiyari.
Waziri wa Ulinzi wa ujerumani ataka jeshi kujiandaa na vita ifikapo 2029
Pistorius ameongeza na hapa ni nukuu yake: "Tunakisia kwamba mfumo unaovutia wa usajili jeshini utawaleta vijana wa kutosha wanaotaka kujitolea wenyewe. Lakini endapo, kwa namna fulani, hali haikuwa hivyo, itabidi uamuzi ufanyike wa ikiwa uandikishaji jeshini unapaswa kuwa wa lazima kwa vijana." Mwisho wa kumnukuu.
Ujerumani ilisitisha uandikishaji wa lazima jeshini na huduma za kiraia mwaka 2011 baada ya miaka 55 ya kuwa na utaratibu huu, na hivyo kuivunja mifumo yote iliyokuwa ikihusiana na utekelezwaji wa sharti hilo.
Sheria ya kuandikishwa kwa wanaume jeshini inaweza kutumika tena
Hata hivyo, sheria inayoruhusu kuandikishwa kwa wanaume iliendelea kubakia na inaweza kuamriwa kutumika tena inapotokezea hali ya dharura.
Pistorius alisema lengo la serikali ni kuanza na mfumo huo mpya wa uandikishaji jeshini ndani ya mwaka huu.
Vyama vya SPD, CDU na CSU vinakubaliana juu ya haja ya kulitanuwa jeshi la Ujerumani, maarufu kama Bundeswehr, sio tu kwenye vikosi vyake vyenye maafisa 180,000 bali pia kwenye askari wake wa akiba.
Hata hivyo, waziri huyo wa ulinzi wa Ujerumani ameonya kwamba Bundeswehr ya sasa haina tena uwezo iliyokuwa nao miaka 30 iliyopita, akitaja upungufu wa vitanda, kambi, wakufunzi na vifaa vyakijeshi.
Kwa mujibu wa Pistorius, makubaliano ya kuunda serikali ya mseto ni fursa ya kuharakisha ununuzi wa vifaa vya kijeshi na miradi ya miundombinu, akibainisha mipango ya kurahisisha upatikanaji wa vibali vya ujenzi wa miradi ya kijeshi na kupunguza urasimu kwenye sekta hiyo ya ulinzi.
Ujerumani kupendekeza hatua ya kuwasajili vijana jeshini
Waziri huyo wa ulinzi amesema kuweka kipaumbele kwenye miradi ya miundombinu ya kijeshi ni muhimu sana kwenye kuimarisha usalama wa taifa na uwezo wa ulinzi, na hivyo miradi hiyo lazima iende haraka ili kuweza kuongeza idadi ya wanajeshi na kuwa na nafasi ya mifumo mipya ya ulinzi.