Ujerumani yatishia hatua dhidi ya Israel kuhusiana na Gaza
27 Mei 2025Merz ametoa matamshi makali na yasio ya kawaida dhidi ya Israel akisema mateso kwa raia wa Gaza hayawezi tena kuhalalishwa kwa hoja ya kupambana na ugaidi wa Hamas. Aliongeza kuwa sasa ni wakati wa kuimarisha mazungumzo na serikali ya Israel ili kuelewa dhima ya operesheni hizo.
Kauli hizi zimeashiria mabadiliko makubwa katika msimamo wa Ujerumani, ambayo kwa muda mrefu imekuwa mshirika wa karibu wa Israel. Katika hotuba yake, Kansela Friedrich Merz alisisitiza kwamba hatua za kijeshi za hivi karibuni haziwezi tena kueleweka kama za kujilinda.
''Ilionekana, na bado naona wakati ulikuwa umefika ambapo nilihitajika kusema hadharani kwamba kinachoendelea huko kwa sasa hakivumiliki tena, na kwa sababu hiyo tutaimarisha mazungumzo na serikali ya Israel,'' alisema Merz katika mkutano na Waziri Mkuu wa Finnland, Petteri Orpo.
Israel yachukulia kwa uzito kauli ya Merz
Kauli za Merz zimepokewa kwa tahadhari kubwa, zikiungwa mkono na baadhi ya wabunge wa mrengo wa kati na kushoto, huku Balozi wa Israel nchini Ujerumani, Ron Prosor, akisema kwamba Israel inasikiliza kwa makini kauli za Merz kwa sababu ni "rafiki wa kweli”. Hata hivyo, alisisitiza kuwa Israel itaendelea na operesheni zake hadi Hamas itakapokoma kuwashambulia Waisraeli na kuwaachilia mateka walioko Gaza.
Msimamo wa Merz umepokelewa kwa tahadhari pia na Baraza Kuu la Wayahudi nchini Ujerumani. Rais wake Josef Schuster amesema ingawa anakubaliana na wito wa kulinda raia na kufikisha misaada Gaza, anatahadharisha dhidi ya kauli ambazo zinaweza kuhalalisha chuki dhidi ya Wayahudi kwa kisingizio cha ukosoaji wa Israel.
Kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa UjerumaniJohann Wadephul amesisitiza kuwa Ujerumani haitalazimishwa kuwa na mshikamano wa kisiasa na Israel pale ambapo haki za binadamu na misaada ya kibinadamu vinaingiliwa. Amesema Ujerumani lazima ifikirie kwa makini hatua zake zijazo kuhusiana na mzozo huo.
Umoja wa Ulaya nao waanza kupaza sauti
Msimamo wa Umoja wa Ulaya pia umeanza kubadilika, huku Rais wa Hamlashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen akilaani mashambulizi ya Israel dhidi ya shule na vituo vya wakimbizi kuwa "ya kutisha na yanayokiuka sheria za kimataifa.” Umoja huo umeshaanza kupitia upya mkataba wake wa ushirikiano na Israel kufuatia mashambulizi haya.
Mashirika ya misaada ya kimataifa yameripoti kuwa zaidi ya watu 180,000 wamehama makazi yao katika kipindi cha wiki moja pekee tangu kuongezeka kwa operesheni za Israel, huku yakielezea wasiwasi kuhusu mfumo mpya wa utoaji misaada unaoungwa mkono na Marekani na Israel, wakisema unadhoofisha misingi ya kibinadamu kwa kutokuwashirikisha Wapalestina na Umoja wa Mataifa.
Katika hatua nyingine, Umoja wa Mataifa umesema hauna uthibitisho wowote kuwa misaada ya chakula inayodaiwa kupelekwa Gaza na shirika jipya la GHF imewafikia wananchi. Mashrika ya UNRWA na OCHA yamesema kiwango cha misaada kinachowasili ni kidogo mno ukilinganisha na mahitaji halisi ya chakula, dawa, na huduma za dharura katika eneo hilo.
Chanzo: dpa, rtre, afpe,ape