Ujerumani yasaka kuungwa mkono EU bajeti ya ulinzi NATO
26 Mei 2025Mkutano wa Finland unatarajiwa kuangazia usalama wa jumuiya ya NATO kutokana na kuongezeka kwa vitisho kutoka Urusi, pamoja na ushirikiano wa kiuchumi.
Merz atahudhuria dhifa ya jioni na mawaziri wakuu wa nchi za Nordic katika kasri la kihistoria mjini Turku, kusini magharibi mwa Finland.
Finland na Sweden ziliingia rasmi NATO baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, hatua iliyochochewa na hofu ya usalama hasa kwa Finland, yenye mpaka wa kilomita 1,340 na Urusi. Ripoti mpya zimeibuka zikionyesha kuongezeka kwa majeshi ya Urusi karibu na mpaka huo.
Mbali na Finland, mkutano huo unawakutanisha pia wawakilishi kutoka Sweden, Norway, Denmark, na Iceland, pamoja na maeneo yanayojitawala ya Greenland na Visiwa vya Faroe (chini ya Denmark), pamoja na kisiwa cha Aland cha Finland.
Ingawa mjadala kuhusu madai ya Rais wa Marekani Donald Trump kutaka kuileta Greenland chini ya udhibiti wa Marekani umetulia kwa sasa, suala hilo linaweza kurejea katika ajenda ya mkutano, likiwa limefungamanishwa na hoja za usalama wa kitaifa na kimataifa.
Waziri Wadephul azuru Hispania na Ureno
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul yuko nchini Hispania na Ureno—wanachama wa NATO wanaotumia kiasi kidogo sana kwa bajeti ya kijeshi—kutafuta uungwaji mkono kwa pendekezo la Ujerumani la kuongeza matumizi ya ulinzi hadi asilimia 3.5 ya Pato la Taifa (GDP), pamoja na asilimia 1.5 zaidi kwa miundombinu ya kijeshi.
Katika ziara yake, Wadephul anakutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Hispania José Manuel Albares mjini Madrid, kisha atasafiri kwenda Lisbon kwa mashauriano na Waziri Paulo Rangel wa Ureno.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, mazungumzo hayo pia yataangazia uhusiano wa nchi hizo mbili, msaada kwa Ukraine, hali ya Mashariki ya Kati na sera ya usalama na ulinzi barani Ulaya.
Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye ameonyesha kuchoshwa na hali ya mataifa ya Ulaya kutegemea bajeti kubwa ya ulinzi ya Marekani, amependekeza kiwango hicho kipande hadi asilimia 5 ya GDP.
Kwa sasa, Hispania inatumia karibu asilimia 1.3 ya pato lake jumla kwa ulinzi – chini sana ya lengo la sasa la NATO la asilimia 2. Ureno, licha ya kuongeza bajeti yake, ilikuwa bado chini ya kiwango hicho kwa kutumia asilimia 1.6 ya pato jumla kufikia mwaka 2024.
Malengo mapya ya matumizi ya kijeshi kwa wanachama wa NATO yanatarajiwa kupitishwa rasmi kwenye mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo mwezi Juni katika jiji la The Hague, Uholanzi.