Ujerumani yasitisha lebo ya itikadi kali dhidi ya AfD
8 Mei 2025Mahakama ya mjini Cologne imesema Alhamisi kwamba shirika la ujasusi wa ndani la Ujerumani, BfV, litasitisha kwa muda kukitangaza chama cha Alternative for Germany (AfD) kuwa kundi la msimamo mkali wa kulia, hadi pale kesi iliyofunguliwa na chama hicho itakaposikilizwa na kuamuliwa rasmi.
Hatua hiyo ya muda inamaanisha kuwa BfV haitaitaja hadharani AfD kama "kundi la msimamo mkali wa kulia lililothibitishwa” mpaka mahakama itoe uamuzi kuhusu ombi la chama hilo la kutaka zuio la muda dhidi ya tangazo hilo.
Tangu wiki iliyopita, BfV ilikuwa tayari imetangaza kuwa AfD — chama kikuu cha upinzani bungeni — ni tishio kwa demokrasia ya Ujerumani, hatua ambayo ingeruhusu shirika hilo kuchukua hatua kali zaidi za kiusalama kama vile kusikiliza mawasiliano ya chama na kutumia wapelelezi wa ndani.
Soma pia: Wajerumani weusi wahofia ushindi wa AFD majimbo ya mashariki
Ripoti ya kurasa 1,100 iliyowasilishwa kwa misingi ya tathmini ya kina (lakini isiyochapishwa kwa umma) ilisema kuwa AfD ni chama kinachochochea ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Waislamu, na kwamba kinaendeleza misimamo inayovuruga hadhi ya utu wa binadamu.
Migawanyiko ya kisiasa yazidi kujitokeza
AfD, kwa upande wake, imelalamika kuwa hatua hiyo ni njama ya kisiasa ya kukidhalilisha chama hicho na kukizuia kushiriki kikamilifu katika siasa za kidemokrasia.
Viongozi wake wawili, Tino Chrupalla na Alice Weidel, wameuelezea uamuzi wa mahakama kama "hatua muhimu ya awali kuelekea kujiondolea lawama” dhidi ya tuhuma za msimamo mkali wa kulia.
Soma pia:Jinsi shambulio la Magdeburg linavyochochea mrengo mkali Ujerumani
Wakati mvutano huu ukiendelea kitaifa, ofisi ya ujasusi ja jimbo la Brandenburg mashariki mwa Ujerumani ilitangaza kuwa tawi la AfD la jimbo hilo limepandishwa daraja kutoka kuwa "linalohisiwa kuwa la msimamo mkali” hadi kuwa "kundi lililothibitishwa la msimamo mkali wa kulia,” kuanzia Aprili 14.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Brandenburg, Katrin Lange, alimkosoa mkuu wa ofisi hiyo, Jörg Müller, kwa kuchelewa kutoa taarifa hiyo kwa umma. Alimfuta kazi Jumanne kwa kile alichokiita "kukosekana kwa uaminifu.”
Tawi la Brandenburg limekuwa la nne kutajwa rasmi kama kundi la msimamo mkali wa kulia, likifuatiwa na yale ya Thuringia, Saxony, na Saxony-Anhalt — majimbo ya mashariki mwa Ujerumani ambako AfD inaungwa mkono kwa kiasi kikubwa.
Wataalamu wanasema mvutano huu unaonyesha changamoto kubwa ya Ujerumani katika kushughulikia vyama vya siasa vyenye misimamo mikali ndani ya mfumo wa kidemokrasia.
Huku serikali mpya ya kihafidhina chini ya Kansela Friedrich Merz ikiingia madarakani, macho yote sasa yameelekezwa kwenye uamuzi wa mahakama kuhusu hatima ya AfD.