Ujerumani yasema hali ya Gaza haivumiliki
4 Agosti 2025Waziri Wadephul ameilaani Israel kwa kile inachofanya kwenye Ukanda wa Gaza na kwamba nchi hiyo inaweza kuwamo katika hatari ya kutengwa kidiplomasia duniani.
Waziri huyo wa Ujerumani kwa mara nyingine ametoa wito wa kusimamisha mapigano mara moja, kwenye eneo la Gaza. Wadephul ameitaka serikali ya Israel kurejesha ushirikiano na Umoja wa Mataifa katika ugavi wa misaada kwa wapalestina huko Gaza.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amefanya ziara kwenye Ukingo wa Magharibi ambako aliionya Israel dhidi ya mpango wa kuinyakua sehemu hiyo.
Pia amelaani mashambulio yanayofanywa na walowezi wa Kiyahudi kwa Wapalestina wa eneo hilo. Wakati huo huo ndege za jeshi la Ujerumani zimeanza kushiriki katika juhudi za kudondosha misaada kwa watu wa Gaza.
Ujerumani ambayo siku zote imekuwa upande wa Israel, ikiwa na Ufaransa na Uingereza zimeongeza miito ya kuitaka Israel kuruhusu misaada ya kiutu iingizwe Gaza mahali ambako Israel inapambana kulisambaratisha kundi la Hamas.