Ujerumani yamfungulia mashtaka raia wa Urusi
20 Agosti 2025Mshukiwa, anayejulikana kwa jina la Akhmad E. kwa mujibu wa sheria za faragha za Ujerumani, alikamatwa tarehe 20 Februari katika uwanja wa ndege wa mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, wakati akijiandaa kupanda ndege. Sasa amefunguliwa mashtaka ya kulisaidia shirika la kigaidi la kigeni, kujaribu kuwa mwanachama wa kundi hilo na kuandaa matukio ya ghasia kubwa.
Waendesha mashtaka wa serikali Kuu walisema kuwa mshukiwa awali alipanga kufanya shambulio nchini Ujerumani, dhidi ya Ubalozi wa Israeli. Inadaiwa alitafuta maelekezo ya kutengeneza vilipuzi mtandaoni, lakini hakufanikisha mpango huo kwa sababu hakuweza kupata vifaa vinavyohitajika.
Hatma ya kesi yake kutolewa baadaye
Wakati huohuo, inasemekana alikuwa akitafsiri propaganda za Dola la Kiislamu IS kwa lugha ya Kirusi na Kichecheni. Waendesha mashtaka walisema alikusudia kujiunga na kundi hilo nchini Pakistan na kupata mafunzo ya kijeshi, na alifadhili safari hiyo kwa kuchukua mikataba ya simu ghali mbili, ambazo baadaye aliuza.
Inadaiwa pia alituma vidio ya kiapo cha uaminifu kwa IS kwa mwananchama mmoja wa kundi hilo nje ya Ujerumani muda mfupi kabla ya kusafiri.
Mashtaka hayo yaliwasilishwa mapema mwezi huu katika mahakama ya Berlin, ambayo sasa itapaswa kuamua kama kesi hiyo itapelekwa mahakamani.