Ujerumani yakosoa hatua za Israel huko Palestina
24 Machi 2025Wasiwasi wa Ujerumani umetokana na kuongezeka kwa mashambulizi ya anga ya Israel yaliyoanza Jumanne wiki iliyopita huko Gaza na kulenga maeneo wenye wakazi wengi. Israel imeanzisha pia operesheni za ardhini na kusambaratisha hali ya utulivu iliyoshuhudiwa kwa muda wa wiki sita kufuatia awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani Christian Wagner amesema ni wazi kwamba ni lazima sasa kurejea haraka kwenye mchakato wa awali wa mazungumzo ya amani akisisitiza kuwa operesheni mpya za kijeshi za Israel hazitowezesha kuachiliwa kwa mateka waliosalia na zitapelekea hali ya kibinadamu kuwa mbaya zaidi huko Gaza.
Ujerumani ambayo kwa kawaida ni mshirika mkubwa wa Israel, imekosoa pia kile ilichokiita kauli zisizokubalika za Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz ambaye wiki iliyopita alitishia kuchukua udhibiti wa baadhi ya maeneo ya Gaza ikiwa Hamas haitowaachia mateka wa Israel waliosalia.
Soma pia: Mataifa ya Ulaya: Mpango wa kusitisha vita gaza urejeshwe
Msemaji huyo wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani amelaani pia uamuzi wa Israel wa kuyatambua zaidi ya makazi kumi na mbili ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, akisema kuwa sera ya upanuzi wa makazi hayo inadhoofisha juhudi za kufikia suluhisho la mataifa mawili. Wagner ameongeza kuwa ikiwa lengo ni kuunda mamlaka ambayo inadhamiria kuwafukuza Wapalestina katika ardhi yao, basi hilo halikubaliki na ni lazima lilaaniwe.
Umoja wa Ulaya watahadharisha kuhusu mashambulizi ya Israel huko Syria na Lebanon
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas ameonya leo wakati wa ziara yake mjini Jerusalem kwamba mashambulizi ya Israel huko Syria na Lebanon yanaweza kupelekea hali kuwa mbaya zaidi katika eneo hilo tangu kufikiwa mwezi Novemba kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran. Aidha Kallas ametoa wito wa kuendelea na mazungumzo katika mzozo wa Gaza.
"Kurejesha mazungumzo kuhusu Gaza, ndiyo njia pekee inayoweza kukomesha mateso ya pande zote. Ghasia huchochea ghasia zaidi. Tunachoshuhudia sasa ni ongezeko la vurugu, linasalobabisha hali ya sintofahamu isiyoweza kuvumilika kwa mateka na familia zao, na vile vile hofu na vifo kwa watu wa Palestina."
Soma pia: Israel yashambulia njia za magendo za kusafirisha silaha kwa Hezbollah
Hayo yakiarifiwa, Misri imependekeza mpango mpya wa usitishwaji mapigano huko Gaza. Shirika la habari la Qatar la Al-Arabi al-Jadid limesema pendekezo hilo limewasilishwa kwa pande zote huku Hamas ikithibitisha kulipokea na Israel ikiwa haijasema chochote.
(Vyanzo: Mashirika)