Ujerumani yakabiliwa na joto la kupindukia
13 Agosti 2025Shirika la utabiri wa hali ya hewa Ujerumani limekadiria viwango vya juu vya joto kufikia nyuzi 37 katika viwango vya Celsius, huku pwani ya kaskazini mwa Ujerumani tu ikitarajiwa kuwa na hali ya joto lisilo la kupindukia.
Wimbi hilo la joto linatarajiwa kuzidi Alhamisambapo nyuzi joto zinatarajiwa kupindukia 38.
Hapo Jumanne, jimbo la kusini magharibi la Baden-Württemberg lililo karibu na mpaka wa Ufaransa, lilirekodi viwango vya juu vya joto vilivyofikia nyuzi 35.4 katika viwango vya Celsius.
Watabiri wa hali ya hewa wametahadharisha kwamba joto hilo bado halijafikia kilele chake.
Kiwango cha joto cha kupitiliza kama hicho husababisha athari za kiafya hasa kwa wazee, wale walio na magonjwa sugu na wafanyakazi wasio na viyoyozi katika maeneo yao ya kazi.
Wataalam wanasema hospitali nyingi na makao ya wazee nchini Ujerumani hayana vifaa vya kukabiliana na joto la kupindukia.