Ujerumani yaishtumu Urusi kwa udukuzi
7 Septemba 2021Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Ujerumani Andrea Sasse amesema kirusi cha udukuzi kinachojulikana kama Ghostwriter, kimekuwa kikikusanya data za kimtandao na propaganda zinazoilenga Ujerumani.
Sasse ameongeza kuwa, kuelekea kwa uchaguzi wa bunge la Ujerumani mnamo Septemba 26, kumekuwa na majaribio kwa kutumia barua pepe miongoni mwa mbinu nyengine za kupata maelezo binafsi ya wabunge.
Soma zaidi: Akaunti ya Twitter ya Obama, Biden zadukuliwa
Msemaji huyo wa wizara ya mambo ya nje amewambia waandishi wa habari na hapa namnukuu, "Hujuma hizi za mtandaoni huenda zikatumika kwa ajili ya kueneza propaganda na kampeni za uwongo kuhusu uchaguzi wa bunge la Ujerumani."
Ameongeza kuwa serikali ya Ujerumani ina habari za kuaminika juu ya mienendo ya kirusi hicho cha udukuzi kinachotambulika kama Ghostwriter, na kwamba kina mafungamano na wadukuzi wa mtandaoni wanaohusishwa na idara ya kijasusi ya Urusi-GRU.
Kirusi cha Ghostwriter kina mafungamano na wadukuzi wa mtandaoni wanaohusishwa na idara ya kijasusi ya Urusi-GRU.
Sasse amesema tabia hiyo inatishia kuupaka tope uhusiano kati ya Urusi na Ujerumani.
"Serikali ya shirikisho ya Ujerumani inaiona hatua hii kama isiyokubalika na hatari kwa usalama, na kwa mchakato wa demokrasia, na pia inatishia kuuharibu uhusiano kati ya nchi hizi mbili. Serikali ya shirikisho ya Ujerumani inaihimiza Urusi kukomesha haraka iwezekanavyo mienendo yake ya udukuzi."
Ameitaka Urusi kukomesha mara moja chokochoko zake, na amewaambia ana kwa ana maafisa wa Urusi katika mkutano wao wa hivi karibuni uliofanyika Alhamisi na Ijumaa. Katika mkutano huo, Naibu Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Miguel Berger, alimuelezea bayana mwenzake wa Urusi juu ya udukuzi huo.
Soma zaidi: Macron apatikana kwenye orodha ya udukuzi
Sasse hata hivyo, hakuelezea zaidi juu ya athari ya udukuzi huo au uharibifu unaoweza kutokea, japo amesema tu kuwa tabia hiyo haikubaliki kamwe na kwamba serikali ya Ujerumani ina haki ya kuchukua hatua zaidi.
Mnamo katikati ya mwezi Julai, mkuu wa idara ya ujasusi wa Ujerumani alisema kuwa, tangu mwezi Februari idara hiyo imeshuhudia ongezeko la majaribio ya udukuzi yanayolenga kuchukua data kutoka akaunti binafsi za wabunge wa Ujerumani na wafanyikazi wao.