Ujerumani yafunga ubalozi wake Sudani Kusini
22 Machi 2025Serikali ya Ujerumani imesema leo kwamba inaufunga kwa muda ubalozi wake nchini Sudani Kusini kutokana na mzozo unaozidi kuwa mbaya katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock katika mtandao wa kijamii wa BlueSky imesema baada ya miaka mingi ya kuwepo kwa hali tete ya kiusalama sasa Sudani Kusini iko mbioni kudumbukia tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Soma zaidi: Mahakama ya Gabon yapitisha majina nane ya wagombea urais
Sudani Kusini ilipata uhuru wake mwaka 2011 kutoka Sudan na muda mfupi baadaye ilidumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na mwaka 2020 Rais Salva Kiir na mpinzani wake Makamu wa Rais Riek Machar waliunda serikali ya pamoja ya mpito lakini kwa sasa uhusiano baina yao unaonekana kuwa mbaya kwa mara nyingine.
Kwa wiki kadhaa sasa wapiganaji wa jamii ya Nuer ambalo ndio kabila la Machar wamekuwa wakipambana na wanajeshi wa serikali katika eneo la mpaka wa nchi hiyo na Ethiopia. Makumi ya watu wameuawa katika mapigano hayo huku pande mbili zikitupiana lawana.