Ujerumani yafanikiwa kuunda serikali ya mseto
9 Aprili 2025Makubaliano hayo yamefikiwa leo baada ya wiki kadhaa za majadiliano kutokana na muungano huo kushinda uchaguzi wa bunge mwezi Februari.
Soma pia:Vyama vya CDU/CSU na SPD vyaanza mazungumzo ya awali ya kuunda serikali
Mara baada ya kufikiwa makubaliano serikali mpya ya Ujerumani imeanza kuangazia changamoto nyingi za kimataifa na za ndani zinazolikabili taifa hilo.
Kansela mteule Friedrich Merz alisema vyama hivyo vitafanya "kwa pamoja kile ambacho Ujerumani inahitaji kwa dharura," na kwamba serikali hiyo ya mseto itakuwa na kauli mbiu ya "mageuzi na uwekezaji."
"Makubaliano ya serikali ya mseto ni ishara ya mwanzo mpya na ishara yenye nguvu kwa nchi yetu. Muelekeo wa kisiasa wa nchi yetu uko katika nafasi ya kutatua matatizo tunayokutana nayo."
"Serikali ya baadaye, serikali ya mseto, itafanya mageuzi na kuwekeza ili kuifanya Ujerumani iendelee kuwa imara, kuwa salama zaidi na kuwa na uchumi imara tena. Na Ulaya pia inaweza kuitegemea Ujerumani."
Soma pia:Ujerumani yaweka hadharani rasimu ya mpango mpya wa matumizi ya fedha
Serikali hiyo mpya inatarajiwa kuimarisha sheria za uraia, na kubatilisha mageuzi ya utawala uliopita, ikiw ani pamoja na kuondoa uwezekano wa kupata uraia wa Ujerumani baada ya kuishi Ujerumani kwa miaka mitatu.