Ujerumani yasitisha kuunganishwa kwa familia za wakimbizi
29 Mei 2025"Kabla sijaingia Ujerumani, sikujua kuwa mambo yangekuwa magumu hivi. Sikutegemea kabisa. Unajua sisi wanaume hatujaandaliwa kulea watoto," alisema Mohammed. Alitoroka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria mwaka 2014 akiwa na mke wake, mabinti wawili na wavulana wawili, na kuelekea Kurdistan ya Iraq.
Maisha yalikuwa magumu sana kwa familia hiyo kiasi kwamba mke wake, mabinti zake wawili na mtoto mmoja walilazimika kurejea Syria. Mohammed, ambaye hakutaka jina lake la familia litajwe, aliamua kuanza safari hatari kuelekea Ujerumani kupitia Libya na Bahari ya Mediterania hadi Italia akiwa na mwanawe mwenye ugonjwa wa kupungua kwa ubongo (cerebral atrophy), akitumaini kupata matibabu na hatimaye kuungana tena na familia yake.
Lakini baada ya miaka miwili na nusu tangu afike Ujerumani, Mohammed bado anaishi peke yake na mwanawe mwenye umri wa miaka 9 na ulemavu mkubwa, bila kujua ni lini au kama mke wake na mabinti zake wataweza kumfuata. Mwanawe wa pili alifariki baada ya kurejea Syria – pigo kubwa ambalo limezidishwa na maumivu ya kutengana.
Mohammed aliwekwa kwenye makazi ya pamoja ya wakimbizi kabla ya rafiki mmoja kumpa hifadhi katika nyumba anayoieleza kuwa ni chakavu. Anasema maisha yao yanategemea msaada wa ustawi wa jamii (social welfare) ambao hautoshelezi mahitaji yao ya kila siku.
Alipofika Ujerumani, mamlaka zilimpa Mohammed hadhi ya ulinzi wa muda (subsidiary protection) – ambayo hutolewa kwa wale wasiokidhi vigezo vya hifadhi ya kisiasa chini ya Mkataba wa Geneva lakini wana hatari ya mateso, adhabu ya kifo au ukatili mkubwa wakirejea nyumbani.
Kwa sasa, takriban watu 351,400 wenye hadhi hiyo wanaishi Ujerumani – wengi wao wakiwa ni raia wa Syria. Wana haki ya kuishi, kufanya kazi na kupata huduma za kijamii. Hata hivyo, tofauti na wakimbizi waliotambuliwa rasmi, watu wenye ulinzi wa muda hawaruhusiwi kuwaleta wake, waume au watoto wao walio chini ya miaka 18.
Serikali mpya yasitisha mpango wa kuungana kwa familia
Mnamo Jumatano, Mei 28, Baraza la Mawaziri la Ujerumani liliidhinisha rasmi kusitishwa kwa muda mpango wa kuungana kwa familia kwa watu wenye hadhi ya ulinzi wa muda. Mswada huo unahitaji kupitishwa na Bunge la Shirikisho (Bundestag) kabla ya kuanza kutekelezwa. Serikali ya muungano inayoundwa na CDU, CSU na SPD imepanga kusimamisha mpango huu kwa angalau miaka miwili ijayo.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Alexander Dobrindt, alisema kuwa uwezo wa nchi kuendeleza ujumuishaji (integration) wa wakimbizi umefikia kikomo. "Majiji na manispaa kote nchini yamezidiwa uwezo," aliongeza.
Tangu mwaka 2018, familia za watu waliopata hadhi ya ulinzi wa muda zimekuwa na fursa ya kuungana nao kupitia visa maalum. Hata hivyo, serikali ya Ujerumani huweka kikomo cha visa 1,000 kwa mwezi – hali ambayo imeleta mkanganyiko mkubwa kwa watu kama Mohammed na familia yake waliobaki Syria.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, mwaka 2024 jumla ya visa 120,000 za kuungana kwa familia zilitolewa, ambapo asilimia 10 pekee (takriban visa 12,000) zilitolewa kwa jamaa wa watu walio na hadhi ya ulinzi wa muda.
Mashirika ya haki za binadamu kama Pro Asyl yameonya kuwa kutengana kwa familia kuna athari kubwa za kisaikolojia kwa wahusika, jambo linalozuia ujumuishaji na kuchochea uhamiaji usio halali. Bila njia rasmi ya kuungana, baadhi ya watu hulazimika kutumia njia hatari za kiharamu kufikia wapendwa wao Ujerumani.
Wataalamu wa sheria wanasema kuwa ingawa sheria za EU hazilazimishi nchi wanachama kuidhinisha kuungana kwa familia za watu wenye hadhi ya ulinzi wa muda, Katiba ya Ujerumani (Ibara ya Sita) na Mkataba wa Haki za Binadamu wa Ulaya zinahakikisha haki ya maisha ya kifamilia.
Lakini Mahakama ya Katiba ya Ujerumani na Mahakama ya Haki za Binadamu Ulaya zimeweka sharti muhimu: ikiwa familia inaweza kuunganishwa katika nchi nyingine, hasa ya asili, basi si lazima kuungana Ujerumani.
Familia zinabaki kugawanyika na mfumo wa kizembe
Mohammed anasema kuwa kutenganishwa na familia yake kumemnyima uwezo wa kujifunza Kijerumani au kufanya kazi, kwa kuwa hana msaada wowote wa kulea mtoto wake mgonjwa. Kibali chake cha ulinzi wa muda kinadumu kwa mwaka mmoja tu, na si hakika kama kitaongezwa – hasa baada ya mahakama moja ya majimbo kuamua kuwa Syria ni nchi salama na hivyo mtu mmoja hakustahili hadhi hiyo.
"Inapaswa kuwa kuna msaada kutoka kwa serikali ili familia yangu iungane nami hapa – huu ni muktadha wa kibinadamu wa kipekee," alisema Mohammed. "Nauliza tu, ni kwa muda gani zaidi nitaweza kustahimili haya yote?"