Wagombea ukansela Ujerumani wachuana kwenye mdahalo
20 Februari 2025Mgombea wa kihafidhina Ujerumani anayepewa nafasi kubwa ya kuwa kansela mpya Friedrich Merz aliutumia mdahalo huo kuwaomba wapiga kura kumpa mamlaka ya kudhibiti uhamiaji haramu na kuujenga upya uchumi. Merz alisema hiyo itasaidia kukimaliza nguvu chama cha siasa kali za mrengo wa kulia AfD.
Katika mdahalo wa mwisho wa televisheni kati yake na Scholz wa siasa za wastani za mrengo wa kushoto kabla ya uchugazi wa Jumapili, Merz alionya kuwa hiyo ndio fursa ya mwisho kusitisha wimbi la chama cha mbadala kwa Ujerumani - AfD. "Tunalazimika kutatua matatizo mawili makubwa kwenye nchi hii katika miaka minne ijayo. Uhamiaji na uchumi. Na tusipotatua matatizo haya mawili, basi nyinyi na sisi na vyama vyote vya kidemokrasia katika ulingo wa siasa hatutakuwa na nafasi katika mabadiliko yajayo ya serikali katika uchaguzi wa shirikisho 2029."
Scholz alisema, kama atachaguliwa tena, ataendeleza juhudi za kuwafukuza wahalifu wa kigeni, lakini pia akasema mashambulizi makali kama lile la gari kuvurumishwa kwenye umati wa watu la wiki iliyopita mjini Munich hayapaswi kuruhusiwa kuigawanya jamii. ''Na pili, wahusika lazima waadhibiwe vikali. Na ikiwa wamefanya makosa kama haya na hawana uraia wa Ujerumani, basi lazima watarajie kwamba tutawarudisha katika nchi nyingine, kuwarudisha katika nchi yao ya asili, kwamba tutatumia mbinu zote na kwamba tutaondoa vizuizi vyote ili kulifanikisha hili.''
Chama cha AfD kinachopinga sera za uhamiaji, kikiungwa mkono vikali na wandani wa Rais wa Marekani Donald Trump, kinaonekana kuwa tayari kupata matokeo bora kabisa ya karibu asilimia 20, kwa mujibu wa tafiti za sasa za maoni ya wapiga kura.
Merz alitoa wito wa kufanywa juhudi kubwa za kurejesha imani ya wapiga kura ili wasiwasikilize wale wanaotaka kuigawa na kuisumbua jamii.
Muungano wa CDU/CSU wa Merz unaongoza katika uchunguzi wa maoni ya wapiga kura kwa karibu asilimia 30, mara mbili zaidi ya uungaji mkono inaopata SPD ya Scholz au chama cha Kijani, lakini kuna uwezekano utahitaji mmoja wao kuwa mshirika wa serikali ya muungano.
Mdahalo huo wa televisheni ya Welt uligusia mada nyingine nyeti kama vile kupanda kwa gharama ya maisha na uchumi wa Ujerumani unaodorora, lakini kwa kiasi kikubwa uliepuka masuala ya sera za kigeni kama vile vita vya Ukraine. Scholz alisema kuwa ''uchokozi wa Urusi dhidi ya Ukraine'' ni moja ya masuala yanayomkosesha usingizi.