Ulaya yaadhimisha miaka 80 ya mwisho wa Vita Kuu ya Pili
8 Mei 2025Ulaya imeadhimisha miaka 80 tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, huku viongozi wa kisiasa wakikumbuka kipindi hicho kama mwanzo wa amani isiyo na mfano barani humo. Hata hivyo, kivuli cha vita kinachotanda sasa nchini Ukraine kimegeuza sherehe za kumbukumbu kuwa ukumbusho wenye maumivu.
Rais wa Bunge la Ulaya, Roberta Metsola, alielezea hali ya sasa kuwa ni sawa na kurudi kwa vita barani Ulaya, akisema: "Miji inalipuliwa tena, raia wanashambuliwa, familia zinatenganishwa. Wananchi wa Ukraine wanapigania si ardhi tu, bali uhuru na demokrasia — kama walivyofanya mababu zetu.”
Kwa Metsola na viongozi wengine, maadhimisho haya hayapaswi tu kuwa ya kumbukumbu, bali pia ya kuchukua hatua kulinda amani, uhuru, na demokrasia ya bara hili.
Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Ujerumani: "Tuna deni kwa walioikomboa Ulaya"
Waziri mpya wa mambo ya nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, amesisitiza jukumu la kihistoria la Ujerumani katika kulinda amani ya Ulaya. Akikumbuka tarehe 8 Mei 1945, alisema: "Siku hii ilibadili historia yetu. Uhuru wetu ni matokeo ya kujitolea kwa majeshi ya Muungano. Kwa hilo, tutadumu kuwa na shukrani.”
Aliongeza kuwa Ujerumani ina wajibu wa kimaadili kutokana na makosa ya enzi ya Manazi na kwamba lazima iendelee kuwa mstari wa mbele kupinga vita na kulinda uhuru barani Ulaya.
Ingawa Ujerumani imekuwa mstari wa mbele kukiri na kuadhimisha makosa ya enzi ya Wanazi, tafiti zinaonesha kuwa maoni ya wananchi yamegawanyika.
Soma pia:
Wafuasi wa chama cha mrengo mkali wa kulia AfD wanaona kuwa historia ya Wanazi inakumbukwa kupita kiasi, ilhali wafuasi wa vyama vya mrengo wa kushoto wanataka historia hiyo ifundishwe na kukumbukwa zaidi.
Putin na Xi wajipambanua dhidi ya "ubabe wa Magharibi”
Katika kilele cha sherehe zao za kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Rais wa Urusi Vladimir Putin alimpokea mwenzake wa China, Xi Jinping, Kremlin. Wawili hao waliapa kulinda "ukweli wa kihistoria” dhidi ya kile walichokiita "ubabe wa mataifa ya Magharibi.”
Soma pia:Viongozi wa Magharibi wakumbuka D-Day chini ya kivuli cha Ukraine
Putin alirudia madai yake ya kuwa vita inayoendelea Ukraine ni mapambano dhidi ya vuguvugu la Wanazi Mamboleo, kauli ambayo imepingwa vikali na mataifa ya Magharibi. Xi naye alisisitiza kuwa China na Urusi zina jukumu la "kupambana na uonevu wa mataifa yenye nguvu.”
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, alikosoa vikali gwaride la kijeshi la Urusi akisema: "Ni gwaride la unafiki. Gwaride la chuki na uongo.” Aliongeza kuwa dunia haina budi kuungana tena kama ilivyofanya miaka 80 iliyopita ili kukabiliana na "uovu” wa sasa wa Urusi.
Zelenskyy aliwataka washirika wa Ukraine kuongeza usaidizi wao kijeshi na wa kidiplomasia ili kuhakikisha amani ya kweli inarudi barani Ulaya.