Ujerumani na Ufaransa wazungumzia uchumi na usalama
29 Agosti 2025Kabla ya kikao hicho kitakachojumuisha mawaziri 10 kutoka pande zote mbili, Merz na Macron walikutana jana Alhamisi jioni katika makaazi ya Macron, Fort de Brégançon.
Baada ya miaka kadhaa ya uhusiano uliokuwa na mvutano na mtangulizi wa Merz, Olaf Scholz, katika mkutano wake na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, rais wa Ufaransa alisema mkutano wake na Kansela Friedrich Merz umeonyesha kwamba mafanikio ya kuanzishwa upya kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili yanaweza kuwa chachu ya kuendesha mchakato wa kuimarisha Ulaya nzima.
"Ninaamini kwamba ushirikiano wa Ufaransa na Ujerumani leo umewekwa sawasawa kabisa kujenga Ulaya yenye nguvu zaidi kiuchumi, kibiashara, kifedha, lakini pia inayodumisha nafasi yake kwenye siasa za ulimwengu katika mzozo wa Ukraine, mbele ya vita vya uvamizi vilivyoanzishwa na Urusi, na Ulaya inayokabiliana na changamoto zake na ambayo imeamua kujihami upya ili kuhakikisha ulinzi wake”, alisema Macron.
Merz pia alisisitiza umuhimu wa uhusiano wa mataifa hayo mawili, akisema: "Ujerumani na Ufaransa zina nafasi ya msingi ndani ya Umoja wa Ulaya, na katika bara zimala Ulaya.”
Mkutano wa pamoja wa baraza la mawaziri
Kansela Friedrich Merz na Rais Emmanuel Macron wataongoza kwa pamoja Baraza la Mawaziri la Ufaransa na Ujerumani mjini Toulon, na baadaye Ijumaa (29.08.2025) Baraza la Ulinzi na Usalama la mataifa hayo litakutana kujadili uzalishaji wa silaha za Ulaya na miradi ya pamoja ya ulinzi.
Mikutano ya aina hii kwa kawaida hufanyika mara moja au mbili kwa mwaka, kwa zamu kati ya Ujerumani na Ufaransa kama wenyeji, ili kuzungumzia usawazishaji wa sera na mipango.
Mara hii mkutano huu unafanyika katikati ya mgogoro wa kisiasa nchini Ufaransa, ambapo Waziri Mkuu Francois Bayrou anatarajiwa kukabili kura ya imani dhidi yake Septemba 8, kura ambayo inaweza kuiangusha serikali yake.