Israel-Iran: Ujerumani na Ufaransa zahimiza diplomasia
20 Juni 2025Jeshi la Israel limesema hivi leo kwamba limeyashambulia maeneo kadhaa mjini Tehran usiku kucha, ikiwa ni pamoja na kile ilichokiita kuwa ni kituo cha "utafiti na maendeleo ya mradi wa silaha za nyuklia wa Iran."
Walinzi wa Mapinduzi wa Iran walisema zaidi ya droni 100 za "vita na kujitoa muhanga" zilirushwa kuelekea Israel siku ya Alhamisi.
Ndege kadhaa za kijeshi za Marekani hazikuonekana tena katika kambi ya jeshi la Marekani nchini Qatar siku ya Alhamisi, kwa mujibu wa picha za satelaiti -- hatua ambayo kuna uwezekano ilichukuliwa kuzilinda dhidi ya mashambulizi ya Iran yanayoweza kutokea.
Katika kile kinachoonekana kama kubadilika kwa kauli yake, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema mabadiliko au kuanguka kwa utawala wa Iran si lengo la operesheni ya kijeshi ya Isreal, lakini inaweza kutokea kama matokeo.
"Lengo letu kuu ni kuuzuia mpango wa nyuklia wa Iran na kuuondoa kabisa kama kitisho. Lengo la pili ni kukomesha, kusitisha na kufuta uwezo wa Iran kutengeneza makombora ya masafa marefu na kuondoa kitisho hicho. Ni wazi tunapofanya hivyo, utawala unadhoofika, lakini suala la kubadilisha utawala liko mikononi mwa watu wa Iran. Hakuna njia ya mkato kuhusu hilo."
Juhudi za kidiplomasia zaendelea
Hayo yakijiri, wanadiplomasia wakuu wa Ulaya wanakutana na waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi mjini Geneva leo kujadili mpango wa nyuklia wa Iran. Mshauri wa Aragchi, Mohammad Reza Ranjbaran, amesema katika taarifa aliyoiandika katika mtandao wa kijamii wa X, kwamba amepokea simu kadhaa zinazomhakikishia utawala wa Kizayuni wa Israel hautamlenga na kumshambulia Araghchi akielekea Geneva.
Aragchi atalihutubia baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa katika mkutano unaoanza leo mchana Geneva. Balozi wa Isreal katika Umoja wa Mataifa Daniel Meron atazungumza na waandishi wa habari kabla mkutano huo kuanza.
Wakati huo huo, mawaziri wa mambo ya nje kutoka Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na Umoja wa Ulaya wanahimiza kusitishwa kwa mzozo huo, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy akisema wiki mbili zijazo ni fursa muhimu ya kufikia suluhu la kidiplomasia, baada ya kukutana na maafisa wa ngazi za juu wa Marekani mjini Washington jana Alhamisi.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani, waziri Lamy na waziri wa mambo ya nje wa Markani Marco Rubio wamekubaliana kwa kauli moja kwamba Iran haiwezi kuruhusiwa kutengeneza na kumiliki bomu la nyuklia.
Kwa upande mwingine, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana leo Ijumaa kwa kikao cha pili kuhusu mzozo huo, kufuatia ombi la Iran ikiungwa mkono na Urusi, China na Pakistan.
Trump kuamua kujiingiza vitani baada ya wiki mbili
Wakati haya yakiarifiwa, Rais wa Marekani Donald Trump alisema Alhamisi ataamua iwapo atajiunga na mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran katika kipindi cha wiki mbili zijazo kwani bado kuna nafasi "kubwa" ya mazungumzo ya kuufikisha mwisho mzozo huo.
Jarida la Wall Street liliripoti kwamba Trump aliwaambia wasaidizi wake alishaidhinisha mipango ya mashambulizi lakini anasita akisubiri kuona kama Iran itaachana na mpango wake wa nyuklia.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekaribisha uwezekano wa Marekani kujiingiza katika kampeni yake ya vita dhidi ya Iran. Lakini Urusi, ambayo ni mshirika wa Iran, imesema hatua yoyote ya kijeshi ya Marekani "itakuwa hatua ya hatari kubwa sana", huku makundi yanayoiunga mkono Iran nchini Iraq yakitishia kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi.