Ujerumani na Nigeria zikubaliana kuimarisha ushirikiano
22 Mei 2025Ujerumani na Nigeria zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wao katika nyanja za uchumi, nishati na uhamiaji. Waziri wa Mambo ya Nje, Johann Wadephul, ameitaja Nigeria kuwa mshirika muhimu wa Ujerumani, barani Afrika.
Wakizungumza baada ya mkutano wao, Waziri Wadephul alisema kuwa ushirikiano na bara la Afrika si muhimu kwa Ujerumani pekee, bali pia kwa bara Ulaya kwa katika siku zijazo. Aliongeza kuwa kuna “fursa nyingi” za kupanua ushirikiano wa kiuchumi na mataifa ya Afrika, akitolea mfano madini adimu yaliyopo kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya bara hilo.
Wadephul pia alieleza dhamira ya kuhamasisha sekta binafsi ya Ujerumani kushiriki kikamilifu nchini Nigeria, akitaja mfano wa kampuni ya magari ya Volkswagen kama kielelezo cha mafanikio.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria, Yusuf Tuggar, alikubaliana na kauli hiyo na kusisitiza kuwa Nigeria tayari ni mshirika wa pili kwa ukubwa wa kibiashara wa Ujerumani katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Tuggar alieleza matumaini ya kukuza zaidi ushirikiano huo, hasa katika sekta ya malighafi muhimu, akisisitiza kuwa Nigeria ina utajiri mkubwa wa madini muhimu.
Katika mazungumzo hayo, Wadephul pia aligusia suala la wahamiaji na wakimbizi wanaovuka Bahari ya Mediterania kuelekea barani Ulaya, hususan Ujerumani.
Nigeria, yenye watu zaidi ya milioni 220, ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika, Kwa mujibu wa Waziri Tuggar, makadirio yanaonyesha kuwa kufikia mwaka 2050, idadi hiyo itafikia milioni 400.
Katika kujibu changamoto ya uhamiaji, serikali ya Nigeria inalenga kuendeleza na kusafirisha vipaji badala ya kuongeza idadi ya wahamiaji, kwa kushirikiana na mataifa kama Ujerumani ili kutafuta suluhisho la ajira na kupambana na uhamiaji haramu.
Uhusiano wa Kihistoria kati ya Ujerumani na Nigeria
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, Berlin inaiona Nigeria kama mshirika muhimu katika kukuza amani, utulivu, na demokrasia katika ukanda mzima wa Afrika Magharibi, sambamba na kuwa taifa lenye uwezo mkubwa wa kiuchumi.
Mnamo Desemba 2023, Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeieralitembelea Nigeria akiwa ameandamana na ujumbe wa wafanyabiashara. Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya shughuli za Tume ya Pamoja ya Ujerumani na Nigeria iliyoanzishwa mwaka 2011. Tume hiyo ina vikundi kazi vinavyoshughulikia masuala ya biashara, nishati, siasa, utamaduni, na uhamiaji, na ilikutana mara ya mwisho mwaka 2021.
Mwaka 2022, hatua ya kihistoria ilichukuliwa kwa kurejeshwa kwa sanamu za shaba za Benin kutoka Ujerumani kwenda Nigeria, jambo lililoashiria mwanzo mpya wa ushirikiano wa kitamaduni kati ya mataifa haya mawili.
Tume hiyo pia inashirikiana katika kupambana na ugaidi, ambapo serikali ya Ujerumani inatoa mafunzo na vifaa kwa vikosi vya usalama vya Nigeria na kuchangia katika miradi ya utulivu wa kimataifa.
Ushirikiano wa Nishati kati ya Ujerumani na Nigeriaulianzishwa mwaka 2008, na uliimarishwa zaidi mwaka 2021 kufuatia uzinduzi wa Mkakati wa Kitaifa wa Hidrojeni wa Ujerumani, ambapo ofisi maalum ya hidrojeni ilifunguliwa mjini Abuja.
Vipaumbele vingine vya ushirikiano wa maendeleo ni pamoja na: maendeleo endelevu ya uchumi, mafunzo ya ufundi, kukuza ajira, maendeleo ya vijijini, upanuzi wa matumizi ya nishati mbadala, na kuboresha huduma za afya.