Ujerumani na Israel: Maadhimisho chini ya kivuli cha vita
12 Mei 2025Mnamo tarehe 12 Mei 1965, Ujerumani na Israel zilianzisha rasmi uhusiano wa kibalozi baada ya kipindi kirefu cha maandalizi. Ilikuwa ni hatua ya kihistoria, ikizingatiwa kuwa wakati huo zilikuwa zimepita miaka 20 tu tangu utawala wa Wanazi wa Ujerumani kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wayahudi wa Ulaya—kumbukumbu ambazo bado zilikuwa mbichi na zenye maumivu katika mataifa yote mawili.
Miaka 80 baadaye tangu mauaji hayo yakomeshwe, uhusiano kati ya Ujerumani na Israel unabaki kuwa wa umuhimu mkubwa—lakini pia wenye changamoto za kihistoria na kisiasa.
Ziara ya kihistoria huku Gaza ikiendelea kuwaka moto
Katika kuadhimisha miaka 59 ya uhusiano huo wa kidiplomasia, Rais wa Israel, Isaac Herzog, anafanya ziara mjini Berlin ambapo ataandamana na mwenyeji wake, Rais Frank-Walter Steinmeier, kutembelea eneo la kihistoria la treni la "Platform 17.” Hapo ndipo maelfu ya Wayahudi walipowekwa kwenye treni na kupelekwa katika kambi za mauaji wakati wa utawala wa Wanazi.
Herzog pia atakutana na vijana wa Kiyahudi kutoka Ujerumani kabla ya kuelekea Israel pamoja na Steinmeier. Wakiwa huko, watazuru kijiji kilichoko karibu na Ukanda wa Gaza—eneo ambalo limekuwa kiini cha vita vinavyoendelea na kuchochea hisia kali dhidi ya Israel duniani kote, ikiwemo hapa Ujerumani.
Katika siku hizi za mwanzo za uongozi wa Kansela mpya Friedrich Merz, uhusiano huu unakabiliwa na changamoto mpya. Merz, kama watangulizi wake, anatambua "jukumu maalum” la kihistoria la Ujerumani kwa Israel—jambo ambalo aliyekuwa Kansela Angela Merkel alilieleza kama "Staatsräson” mwaka 2008, yaani jukumu ambalo ni la kipaumbele cha kiusalama kwa taifa la Ujerumani.
Soma pia: Ujerumani: Mzozo kuhusu hati ya kukamatwa kwa Netanyahu
Ni kwa msingi huo ndipo licha ya ukosoaji mkubwa dhidi ya hatua za kijeshi za Israel huko Gaza, Ujerumani bado inasimama imara na Israel tangu shambulio la Hamas la tarehe 7 Oktoba 2023. Hamas inachukuliwa kuwa kundi la kigaidi na Ujerumani, Umoja wa Ulaya na Marekani.
Mashaka ya kisiasa na kisheria yajitokeza
Hata hivyo, sauti za ukosoaji dhidi ya Israel zimeanza kuongezeka nchini Ujerumani, hususan miongoni mwa vijana. Katika mahojiano yake ya kwanza akiwa Kansela, Friedrich Merz aliiambia runinga ya kitaifa ya ARD kuwa Israel inapaswa kuheshimu sheria za kimataifa.
"Kwetu, Israel ina nafasi ya kipaumbele. Waziri wa Mambo ya Nje ataitembelea nchi hiyo wikendi ijayo. Sitaki kusema zaidi kwa sasa, lakini pia serikali ya Israel lazima itekeleze majukumu yake chini ya sheria ya kimataifa. Inapaswa kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza."
Changamoto nyingine katika uhusiano wa sasa ni suala la hati ya kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ambako Ujerumani ni mwanachama mwanzilishi. Kisheria, Ujerumani inawajibika kumkamata Netanyahu endapo ataingia nchini humo.
Soma pia: Netanyahu asema Israel itajiamulia yenyewe masuala yake ya usalama
Hata hivyo, siku moja baada ya uchaguzi mkuu wa Ujerumani mwezi Februari, Merz alimpigia simu Netanyahu na kusema kuwa kama atakuwa Kansela, atatafuta njia ya kisheria itakayomwezesha kiongozi huyo wa Israel kuzuru Ujerumani bila kukamatwa. Tangu aingie madarakani, Merz hajatoa tamko lolote tena kuhusu suala hilo.