Ujerumani mabingwa wa dunia wa hoki
18 Septemba 2006
Hertha Berlin wamemsangaza jana kila mmoja kwa kutwaa usukani wa Bundesliga-Ligi ya Ujerumani baada ya kuizaba Schalke mabao 2:0.mshambulizi wa argentina Christian Gimenez alitia bao kila kipindi kuipachika Hertha Berlin kileleni ilikokuwapo nüremberg.
Hii ni mara ya kwanza kwa Berlin kujiokuta kileleni mwa Ligi tangu desemba 2000.Schalke kwa kweli, ingeliweza binafsi kuparamia kileleni mwa Ligi laiti ingelishinda jana na sasa imeangukia nafasi ya 6 ya ngazi ya Bundesliga.
Katika mpambano mwengine wa hapo jana Eintracht Frankfurt iliilaza Leverkusen kwa mabao 3-1.Na hii inafuatia ushindi mwengine wa mabao 4:0 dhidi ya brondy katika kombe la Ulaya la UEFA.
Mabingwa watetezi Bayern Munich walikiona kilichomtoa kanga manyoya walipokandikwa mabao 2:1 jumamosi na Armenia Bielefeld.
Rifu aliechezesha changamoto kati ya Alemannia Aachen na Borussia Mönchengladbach alitishia juzi kusimamisha mpambano huo wa bundesliga ikiwa baadhi ya mashabiki uwanjani hawangeacha matusi yao ya kibaguzi.
Rifu Michael Weiner aliwaonya mashabiki kupitia kikuza sauti kwamba angesimamisha mchezo ikiwa maneno kama vile “ wasaka ukumbizi” yakisikika tena uwanjani.Matamshi hayo yakilengwa mchezaji mweusi wa kibrazil anaeichezea Mönchengladbach.
Wiki iliopita, mchezaji wa timu ya taifa wa asili ya Ghana, Gerlad Asamoah ,ambae ni mweusi alitukanwa kwa matusi ya kikabila wakati wa mechi ya kuania kombe la shiriklisho la Ujerumani akiichezea Schalke.Ijumaa iliopita ,shirikisho la dimba la ujerumani liokaipiga faini ya Euro 20,000 Hansa Rostock kwa madhambi hayo ya mashabiki wake.
Katika Premier League-Ligi ya Uingereza,stadi wa ivory Coast,Didier droga aliipatia Chelsea bao la ushindi dhidi ya Liverpool wakati Arsenal imeizima Manchester united pia kwa bao 1:0.Chelsea ilimuona Michael ballaci,nahodha wa Ujerumani akitimuliwa nje na rifu kwa kucheza ngware.
Katika changamoto za kombe la la COSAFA kusini mwa Africa,Angola imeshaweka miadi ya finali mwezi ujao na zambia kwa mara ya 4 baada ya kuikumta Zimbabwe jana mabao 2:1 mjini Harare.
Finali na Zambia itakua Oktoba 21 mjini Lusaka.Angola ikicheza na wachezaji 4 tu waliotamba katika Kombe la dunia hapa ujerumani waliufumania kwanza mango wa Zimbabwe muda mfupi tu kabla kipindi cha pili.
Zimbabwe ambayo imeshinda pia mara tatu kombe la COSAFA la kusini mwa Africa, ilisawazisha mnamo dakika ya 64 ya mchezo pale Francio Candida alipowasangaza wa Angola.Huu ni ushindi wapili mfululizo kwa timu ya taifa ya angola tangu kurudi kutoka Kombe la dunia,Ujerumani.
Wakati Itali jana ilitawazwa mabingwa wa Kombe la Tennis la Federation Cup, Ujerumani ilitawazwa kwa mara ya pili mabingwa wa dunia wa hoki ya uwanjani-field hockey.Ujerumani iliizaba Australia mabao 4-3 baada ya Australia kuongoza kwa mabao 2:0 huko Mönchengladbach.
Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani ya dimba, Jürgen klinsmann alimtaka kocha wa timu ya taifa ya hoki Bernhard Peters awemo katika timu yake ya makocha ili kuisaidia Ujerumani kutwaa kombe la dunia.DFB-shirikisho la kabumbu la Ujerumani lilikataa na sasa ameibuka na timu ya taifa ya Hoki mabingwa wa dunia.
Mashindano ya Kombe la riadha la dunia yalimalizika jana mjini Athens,Ugiriki kwa ushindi wa timu ya bara laUlaya na Urusi kutoroka na taji la timu spande wa wanaume na wanawake:
Msisimko lakini uliletwa uwanjani na mzaliwa wa Kenya, raia wa Qatar,Saif Shaheen.Akikimbia kwa niaba ya bara la Asia,Shaheen, zamani steven Cherono, alichomoka kwa kasi na kunyakua taji la mita 3000 kuruka viounzi kuongezea na lile la masafa ya mita 5000 walilonyakua jumamosi.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa bara la Ulaya kunyakua nafasi ya kwanza spande wa wanaume tangu 1981 na Urusi kutetea taji la wanawake.Zikisalia mita 300, Shaheen alichomoka kwa kasi kama kombora na kumpita mkenya Koech.
Katika mbio za mita 3000 Craig Morttram wa Marekani, alitetea taji lake la masafa hayo kwa kumpiku muethiopia Kenenisa Bekele.
Wakati bara la Afrika ambalo mara nyingi likitamba katika kombe hili la dunia la riadha, mara hii halikufua dafu, bara la Asia, limefanya uziri katika medani ya riadha mara hii:Asia imemaliza 4 kwa mara ya kwanza.