Ujerumani kutoa mchango euro milioni 10 kwa Benki ya Dunia
17 Julai 2025Ujerumani itatoa mchango wa awali wa euro milioni 10 kwa Benki ya Dunia mwaka huu kama msaada wa mpango wa uwekezani barani Afrika wa nchi zilizostawi na zinazoinukia kwa kasi kiuchumi duniani za G20.
Hayo yamesemwa hivi leo na Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Lars Klingbeil mjini Durban nchini Afrika Kusini, siku ya kwanza ya mkutano wa siku mbili wa mawaziri wa fedha wa nchi za G20 unaofanyika huku kukiwa na changamoto ya shinikizo la kiuchumi, hasa kwa uchumi wa nchi za Afrika.
Klingbeil amesema wameshawishika huu ni uwekezaji mzuri na watafurahi sana kuona wanachama wengine wa kundi la G20 wakijiunga nao.
Kabla ya mkutano huo Klingbeil alisema wanataka kujenga ushirikiano wa karibu wa kiuchumi na nchi za Afrika kwa kuzingatia hali ya sintofahamu inayoukabili ulimwengu pamoja na migogoro ya kibiashara.