Ujerumani kusajili wanajeshi wapya
11 Aprili 2025Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius, serikali inasubiri tu kukamilika kwa taratibu za kisheria, ili ianze usajili na mafunzo kwa sehemu ya kwanza ya makuruta wapya 5,000 wanaotazamiwa kujiunga mwaka huu.
Mwanasiasa huyo kutokea chama cha Social Democrat (SPD) alisema kazi ya awali tayari imeshakamilika kwa miezi kadhaa sasa, na hivyo kuziwezesha hatua nyengine kufuata mara tu serikali mpya itakapoanza kazi.
Soma zaidi: Ujerumani yatoa wito kwa vijana wajiunge na jeshi
Makubaliano ya uundaji wa serikali ya mseto kati ya SPD na muungano wa vyama vya kihafidhina vya CDU-CSU yanataka uanzishwaji wa mfumo wa usajili wa jeshini, ambao katika hatua za awali utakuwa wa hiyari.
"Tunakisia kwamba mfumo unaovutia wa usajili jeshini utawaleta vijana wa kutosha wanaotaka kujitolea wenyewe. Lakini endapo, kwa namna fulani, hali haikuwa hivyo, itabidi uamuzi ufanyike wa ikiwa uandikishaji jeshini unapaswa kuwa wa lazima kwa vijana." Alisema Pistorius.
Kurejea kwa uandikishaji wa lazima jeshini
Ujerumani ilisitisha uandikishaji wa lazima jeshini na huduma za kiraia mwaka 2011 baada ya miaka 55 ya kuwa na utaratibu huu, na hivyo kuivunja mifumo yote iliyokuwa ikihusiana na utekelezwaji wa sharti hilo.
Hata hivyo, sheria inayoruhusu kuandikishwa kwa wanaume iliendelea kubalia na inaweza kuamriwa kutumika tena inapotokezea hali ya dharura.
Soma zaidi: Uingereza na Ujerumani kuimarisha ushirikiano wa ulinzi
Pistorius alisema lengo la serikali ni kuanza na mfumo huo mpya wa uandikishaji jeshini ndani ya mwaka huu.
Vyama vya SPD, CDU na CSU vinakubaliana juu ya haja ya kulitanuwa jeshi la Ujerumani, maarufu kama Bundeswehr, sio tu kwenye vikosi vyake vyenye maafisa 180,000 bali pia kwenye askari wake wa akiba.
Udhaifu wa Bundeswehr
Hata hivyo, waziri huyo wa ulinzi wa Ujerumani alionya kwamba Bundeswehr ya sasa haina tena uwezo iliyokuwa nao miaka 30 iliyopita, akitaja upungufu wa vitanda, kambi, wakufunzi na vifaa vya kijeshi.
Kwa mujibu wa Pistorius, makubaliano ya kuunda serikali ya mseto ni fursa ya kuharakisha ununuzi wa vifaa vya kijeshi na miradi ya miundombinu, akibainisha mipango ya kurahisisha upatikanaji wa vibali vya ujenzi wa miradi ya kijeshi na kupunguza urasimu kwenye sekta hiyo ya ulinzi.
Soma zaidi: Jenerali jeshi la Ujerumani ataka wanawake watumikie jeshi
Waziri huyo wa ulinzi amesema kuweka kipaumbele kwenye miradi ya miundombinu ya kijeshi ni muhimu sana kwenye kuimarisha usalama wa taifa na uwezo wa ulinzi, na hivyo miradi hiyo lazima iende haraka ili kuweza kuongeza idadi ya wanajeshi na kuwa na nafasi ya mifumo mipya ya ulinzi.